Header Ads Widget

KAWETIRE YAVUMA: WATU WADUNGWA NA NYUKI KWA TIBA, BODI YA UTALII YASISIMKA NA UBUNIFU HUO.


Katika hali isiyozoeleka lakini yenye mvuto wa kipekee, wananchi na wageni wamefurahishwa na huduma ya  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS inayotolewa  katika Shamba la Miti Kawetire lililopo mkoani Mbeya kwa ajili ya kuhudumiwa na nyuki, wakidungwa makusudi kwa lengo la kupata faida za kiafya, huku hatua hiyo ikitajwa kuwa sehemu ya vivutio vipya katika kukuza utalii wa tiba asilia nchini.

Afisa Nyuki katika shamba hilo, Agnetha Luoga, amesema zoezi hilo la kudungwa na nyuki limekuwa likifanyika kwa hiari ya mtu binafsi, ambapo anaelekezwa kisha kuruhusiwa kudungwa katika maeneo maalum ya mwili ili kusaidia mzunguko wa damu, kuondoa maumivu ya viungo, pamoja na kuamsha kinga ya mwili.

“Nyuki wanapodunga, hutoa sumu ya asili iitwayo melittin ambayo huchochea mfumo wa kinga ya mwili. Watu wenye changamoto kama baridi yabisi, maumivu ya mgongo, au viungo hupona kwa njia hii. Hili ni jambo la kiafya na linafanyika kwa uangalifu mkubwa,” amesema Agnetha Luoga.

Kwa upande mwingine, hatua hiyo imevutia pia sekta ya utalii. Hozza Mbura, Afisa Utalii Mwandamizi ambaye pia ni Mkuu wa Kanda wa Bodi ya Utalii – Nyanda za Juu Kusini, amesema matumizi ya nyuki kama sehemu ya tiba na kivutio cha utalii ni ubunifu unaopaswa kuungwa mkono, kwani unaongeza wigo wa utalii wa kipekee (niche tourism) nchini.

“Tunaona namna wananchi wanavyohitaji kudungwa, lakini pia wanapata nafasi ya kujifunza kuhusu maisha ya nyuki, umuhimu wao katika mazingira na tiba.

 Hili ni jambo ambalo linaweza kuingizwa rasmi kwenye bidhaa za utalii wa tiba (health tourism),” alisema Hozza Mbura.

Wananchi waliodungwa na nyuki nao wametoa maoni mbalimbali, wengi wakieleza walivyojionea nafuu katika miili yao. Esther Mwakyusa, mkazi wa Uyole alisema:

“Nilikuwa na maumivu ya muda mrefu kwenye goti, baada ya kudungwa mara mbili nimeanza kuona mabadiliko. Nilihofia sana, lakini kumbe si kitu cha kuogopa – ni kama sindano tu.”

John Mwakipesile naye aliongeza kuwa:

“Ni jambo la ajabu lakini la kweli, watu wanaweza kuja kutibiwa kwa nyuki na kwa wakati huohuo kutalii – unajifunza na unatunzwa afya.”

Kwa sasa, zoezi hilo linafanyika kwa kufuata taratibu za kiafya, likisimamiwa na wataalamu waliobobea kwenye masuala ya nyuki. Pia, mamlaka za utalii zimeanza kuliona eneo hilo kama fursa ya uwekezaji na elimu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI