Header Ads Widget

NEMC YAFURAHISHWA NA MWITIKIO WA WANANCHI MAONESHO YA NANE NANE MBEYA.

 

Na Matukio Daima Media ,Mbeya

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini limeeleza kuridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi waliotembelea banda lao katika maonesho ya kilimo ya Nane Nane yaliyofanyika jijini Mbeya.


Akizungumza na vyombo vya habari katika viwanja vya John Mwakangale, Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Milton Patrick Mponda amesema wananchi wengi walifika kupata elimu kuhusu hifadhi ya mazingira, huku wakionesha kiu ya kutaka kujifunza zaidi.


“Tumeona mwitikio mzuri wa wananchi mwaka huu, wamekuwa na maswali mengi, wameonyesha kupokea elimu kwa uzito mkubwa, hasa kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na namna bora ya kutunza mazingira katika shughuli zao za kila siku,” amesema Mponda.


Ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, wamepata nafasi ya kutoa elimu kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, usimamizi wa taka ngumu, matumizi ya plastiki, na njia za kilimo rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuifanyia kazi kwenye maisha yao ya kila siku.


“Sikuwa najua kuchoma taka ovyo inaweza kuharibu mazingira kiasi hiki, nimejifunza mengi sana,” amesema Neema Mwakyoma mkazi wa Mbeya Mjini.


“Wametufundisha kuhusu kutunza miti na vyanzo vya maji. Hii ni elimu muhimu sana kwa jamii yetu,” ameongeza msikilizaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la George Mwaitenda Muasisi Wa Mchezo Wa Jogging Mkoa Wa Mbeya 

Maonesho ya Nane Nane kwa mwaka huu yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sekta ya kilimo, mazingira, na maendeleo endelevu, huku NEMC ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kila mmoja kuwa mlinzi wa mazingira.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI