Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa mkoa Kigoma Balozi Simon Siro amewataka wadau wa siasa na uchaguzi mkoani Kigoma kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuwezesha uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uwe wa haki na Amani.
Balozi Siro alisema hayo alipotembelea ofisi ya CCM mkoa Kigoma na kukutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa Kigoma ambapo alisema kuwa lazima watekeleza maelekezo ya Rais Samia kwa pamoja ili kuwezesha uchaguzi kufanyika kwa Amani na usalama.
Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa hakuna mahali ambapo viongozi wazuri ambao wananchi wanawataka wanaweza kupatikana katika hali ya vurugu na vita hivyo ili kuwapa wananchi hao yao ni lazima masuala ya ulinzi na usalama yazingatiwe haki ikiwa msingi mkuu wa mambo hayo.
Kiongozi huyo alisema kuwa ameanza kwa kutembelea ofisi ya CCM na kukutana na kamati ya siasa ya mkoa lakini pia atafanya ziara kwenye vyama rafiki na kukutana na viongozi wote wa vyama hivyo ili kuweka mustakabali mzuri wa kufanya uchaguzi katika hali ya Amani inayozingatia haki kwa wadau wote.
Awali akizungumza katika ziara hiyo ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM,Abdulkadri Mushi alimkaribisha kiongozi huyo mkoani Kigoma na kumuhakikishia kwamba CCM ipo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa Amani,utulivu na kuzingatia haki.
Mushi alisema kuwa kuvurugika kwa Amani siyo jambo la mtu mmoja hivyo wao kama chama wamejikita katika kusimamia Amani na utulivu wa nchii ambayo ni moja ya tunu za taifa na kwamba wana hakika uchaguzi utafanyika kwa Amani na usalama kwa misingi yote ya Katiba na sharia za nchi.
0 Comments