Jeshi la Israel linasema limeanza "hatua za awali" za mashambulizi ya ardhini yaliyopangwa kuuteka na kukalia kwa mabavu mji wote wa Gaza na tayari wameshikilia viunga vyake.
Msemaji wa jeshi alisema kuwa wanajeshi tayari wanaendelea kupanga mikakati yao katika maeneo ya Zeitoun na Jabalia ili kuweka msingi wa mashambulizi hayo, ambayo Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliidhinisha siku ya Jumanne na yatajadiliwa kwenye baraza la mawaziri la usalama baadaye wiki hii.
Takriban wanajeshi wa akiba 60,000 wameitwa kuanzia mwanzo wa Septemba ili kuwaachilia walio kazini kwa ajili ya operesheni hiyo.
Hamas imeishutumu Israel kwa kukwamisha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya kuendeleza "vita vya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia", shirika la habari la Reuters liliripoti.
Mamia kwa maelfu ya Wapalestina katika mji wa Gaza wanatarajiwa kuamriwa kuhama na kuelekea kwenye makazi kusini mwa Gaza huku matayarisho ya Israel yakiendelea.
Washirika wengi wa Israel wamelaani mpango huo, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akionya Jumatano kwamba "unaweza tu kusababisha maafa kwa wote wawili na hatari ya kulitumbukiza eneo lote katika mzunguko wa vita vya kudumu".
Wakati huo huo, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema kuhamisha watu zaidi na kuongezeka uhasama kuna "hatarisha kuzidisha hali ambayo tayari ni janga" kwa wakazi milioni 2.1 wa Gaza.
Serikali ya Israel ilitangaza nia yake ya kuliteka eneo lote la Ukanda wa Gaza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka kusambaratika mwezi uliopita.
0 Comments