Header Ads Widget

VETA KAGERA YAONA MATUNDA YA KAULI YA WAZIRI MKUU,VIJANA WASHAULIWA KUCHANGAMKIA FURSA.


Na Shemsa Mussa -Matukio daima Kagera

Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Kagera kimeanza kuona mafanikio ya utekelezaji wa kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliyewataka vijana nchini kujikita katika mafunzo ya ufundi ili kujiajiri na kuchochea maendeleo ya taifa. Mafanikio hayo yanaonekana kupitia ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi na mwamko mkubwa wa vijana kujifunza fani mbalimbali za ufundi stadi.

Akizungumza na mwandishi wetu, Kaimu Mkuu wa chuo Cha VETA Mkoa wa Kagera Bw Athuman Shaban Mussa, amesema kuwa baada ya kauli hiyo ya Waziri Mkuu, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaojiandikisha katika chuo hicho kwa mwaka huu, ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Amesema vijana sasa wanatambua kuwa mafanikio hayatokani tu na elimu ya darasani bali pia kupitia maarifa ya mikono na ubunifu.

“Tumeshuhudia ongezeko la kujiandikisha na kuchukua fomu kwa asilimia kubwa ya wanafunzi waliodahiliwa mwaka huu. Hii ni ishara kuwa vijana wameuchukua kwa uzito wito wa serikali wa kushiriki katika mafunzo ya ufundi. Tumeongeza kozi mpya ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na ubunifu wa vijana,” amesema Bw Athuman.


Kwa mujibu wa kaimu Mkuu huyo, amezitaja baadhi ya fani zinazotolewa na Veta Kagera  ikiwemo useremala, umeme wa majumbani, udereva wa Magari,uchomeleaji wa vyuma na uashi,pamoja na uhaziri ,Aliongeza kuwa fani hizo zimekuwa zikiwasaidia wahitimu kujiajiri mara tu baada ya kuhitimu masomo yao, huku wengine wakianzisha vikundi vya uzalishaji na biashara ndogondogo.

Aidha, amesema kuwa chuo hicho kimekuwa kikishirikiana na sekta binafsi na halmashauri katika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, jambo ambalo limeongeza ujuzi wa moja kwa moja kazini. Pia alisema kuwa baadhi ya kampuni na taasisi zimekuwa zikiwachukua wahitimu wa VETA Kagera kwa ajili ya ajira kutokana na ubora wa mafunzo wanayopata.

Vijana walioko mitaani wametakiwa kuchangamkia fursa zinazotolewa na VETA kwa kuwa zinawapa msingi imara wa kujitegemea na kuepuka utegemezi. Alisema kuwa chuo kimeendelea kutoa elimu ya stadi kwa gharama nafuu na hata kusaidia baadhi ya vijana wasio na uwezo kwa kushirikiana zaidi  na Serikali.

 PiaVeta Kagera imepanga kuanzisha na kuboresha  programu za mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali waliopo kwenye sekta isiyo rasmi ili kuwaongezea maarifa ya biashara, uendeshaji wa miradi na matumizi ya teknolojia rahisi. Lengo ni kuhakikisha kila kijana mwenye ari ya kujifunza na kubadili maisha yake anapata nafasi.


 Kwa ujumla, VETA Kagera imeendelea kuwa mfano wa mafanikio ya utekelezaji wa maono ya serikali ya awamu ya sita kuhusu ajira kwa vijana. Kaimu Mkuu wa Veta  amesisitiza kuwa endapo vijana watachangamkia kwa bidii fursa hizo, taifa litakuwa na nguvu kazi mahiri, yenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ngazi zote.

Lakini pia Nilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya  vijana wanaosomea fani tofauti tofauti katika chuo cha VETA kata ya  Rwamishenye na kata ya Burugo akiwemo Anitha Amos,Pius Kurwa na Kelvin Chrophas, walionesha hali na bidii kubwa katika taaluma zao,Walielezea jinsi mafunzo ya ufundi yanavyowapa ujuzi wa moja kwa moja unaohitajika kwenye soko la ajira, pamoja na uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Vijana hao walisisitiza kuwa kuna dhana potofu miongoni mwa jamii kuwa wanaoenda  VETA ni wale waliofeli masomo au maisha kwa ujumla, Walikemea mtazamo huo na kueleza kuwa mafanikio hayategemei daraja la shule pekee, bali juhudi binafsi, ubunifu na maarifa sahihi.

Waliwasisitiza vijana wenzao wajikite katika kujifunza ujuzi wa vitendo na waache kusubiri ajira za ofisini pekee,Kwa kupitia VETA, vijana wengi wameweza kuanzisha shughuli zao na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira nchini.

Hata hivyo Mpaka Sasa Mkoa wa Kagera unavyo vyuo vya Veta vinne katika Halmashauri za Muleba,karagwe na Bukoba huku Ujenzi wa vyuo vingine ukiendelea Katika Halmashauri za Missenyi,Kyerwa,Biharamlo na Ngara.                        

 



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI