Header Ads Widget

SINGIDA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA AFYA NA ELIMU – RC DENDEGO

 


Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media  Dodoma

Mkoa Singida imeendelea kuimarika katika utoaji wa huduma za jamii, hususan sekta ya afya na elimu, kufuatia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4 ,2025 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa miradi pamoja na ushirikiano kati ya serikali na wananchi.

Amesema katika sekta ya afya, mkoa umeongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma kutoka 203 mwaka 2020/21 hadi 302 mwaka 2024/25. Kati ya vituo hivyo, zahanati zimeongezeka kutoka 173 hadi 246 na vituo vya afya kutoka 25 hadi 42.


Aidha, hospitali mpya za wilaya tano zimejengwa huku hospitali tatu zikifanyiwa ukarabati mkubwa. Majengo ya huduma za dharura manne na huduma za wagonjwa mahututi matatu yamekamilika, sambamba na vituo vitatu vilivyoboreshwa kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

"Kuna mitambo miwili ya kuzalisha hewa ya tiba aina ya oxygen imewekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mandewa, hatua iliyoongeza uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa mahututi," Amesema . 

" Jumla ya watoa huduma wa afya wamefikia 2,748, ambapo ajira mpya 634 zimetolewa na watoa huduma 193 wamepelekwa mafunzoni kuongeza ujuzi,". 

Ameeleza  kuwa Wastani wa upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 93 huku utoaji wa chanjo ukifikia asilimia 102. Huduma za kibingwa, zikiwemo tembezi na za kudumu, zinaendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa.

Kwa upande wa elimu, shule mpya 142 za msingi zimejengwa, sambamba na shule 40 mpya za sekondari na shule saba za amali. Vyuo vinne vya ufundi stadi (VETA) vinajengwa na kimoja kimekamilika. 


"Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 48 katika utekelezaji wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari huku utoaji wa chakula mashuleni umefikia asilimia 95 na kiwango cha utoro kwa wanafunzi kimepungua kwa kiasi kikubwa," Amesema.

Aidha amesema, vyuo vya utumishi wa umma na uhasibu katika mkoa huo vimeimarishwa kwa kuongeza miundombinu na vifaa vya kufundishia ili kukuza ubora wa elimu ya juu.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa juhudi hizi ni sehemu ya dhamira ya serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na za uhakika, huku akisisitiza kuwa Singida inaendelea kusonga mbele kwa kasi katika kuboresha maisha ya wananchi wake.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI