Header Ads Widget

TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI YAWAASA WARATIBU KUZINGATIA SHERIA NA KATIBA

Na Rehema  Abraham Kilimanjaro 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka waratibu wa uchaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zinazosimamia mchakato wa uchaguzi nchini.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu, wakati wa maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi, yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar, alisema,

 “Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Tume lazima zifuatwe ipasavyo. Hatuwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki kama watendaji wetu hawazingatii misingi ya kisheria.”

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Staslaus Mwita, alisisitiza umuhimu wa watendaji hao kuwa huru kisiasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa haki. Alisema:

“Sheria zipo wazi kuwa msimamizi au mratibu wa uchaguzi hapaswi kuwa mfuasi wa chama chochote cha siasa. Hii ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa anatekeleza majukumu yake kwa uadilifu na bila upendeleo.”

Nao waratibu wa uchaguzi kutoka mikoa ya Tanga na Kilimanjaro ambao walikuwa miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Jasper Ijiko na Sebastian Masanja, walionesha matumaini yao ya kuimarisha utekelezaji wa uchaguzi baada ya mafunzo hayo. Walisema:


 “Baada ya mafunzo haya, tuko tayari kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na uhuru. Tumejifunza mambo mengi yatakayotusaidia kufanya kazi kwa weledi,” alisema Jasper Ijiko.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha washiriki kutoka mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, huku kaulimbiu ya uchaguzi wa mwaka huu ikiwa ni “KURA YAKO, HAKI YAKO – JITOKEZE KUPIGA KURA.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI