Na Mwandishi Wetu, Songwe.
CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kimetangaza rasmi kuwa kitamtangaza mgombea wake wa urais kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 mnamo Agosti 4, 2025.
Tangazo hilo limetolewa , Julai 15, 2025 na Naibu Katibu Mkuu CHAUMA (Tanzania Bara), Benson Kigaila, wakati wa kikao na wanachama wa chama hicho katika Ukumbi wa Hekima Motel mjini Vwawa, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku mbili ya ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi.
Kitendo cha chama hicho kutangaza tarehe rasmi ya kumtangaza mgombea wake wa urais kutamaliza uvumi wa muda mrefu kuwa huenda aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ndiye anayetarajiwa kupeperusha bendera ya CHAUMA.
Hata hivyo, Mbowe mwenyewe hajawahi kuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo.
Kigaila pamoja na mambo mengine, alifafanua kuhusu ushiriki wa CHAUMA katika uchaguzi mkuu ujao, akieleza kuwa chama hicho kitashiriki uchaguzi bila kujali mazingira, huku akitaja sababu kuu tatu zilizofanya chama hicho kushiriki kwenye uchaguzi huo.
"Kwanza, ni wajibu wa kila chama cha siasa kushiriki uchaguzi kwa sababu ndicho chombo cha kidemokrasia cha kuchukua dola na kuleta mabadiliko, kwani chama kisichoshiriki uchaguzi hakina uhalali wa kulalamika," alisema Kigaila.
Sababu ya pili, alisema ni dhamira ya CHAUMA kushinda uchaguzi ili kushughulikia kero za wananchi ambazo serikali ya sasa imeshindwa kuzitatua.
Alitaja changamoto kama wanawake kukosa mikopo, akina mama kukosa huduma bora za afya na mfumo wa elimu usioleta ajira kama baadhi ya matatizo yanayowakabili wananchi.
"CHAUMA inataka kushinda ili kuleta mawazo mapya ya uongozi baada ya CCM kushindwa kutoa mwelekeo mpya licha ya kushika dola tangu mwaka 1961," alisisitiza.
Kigaila alisema sababu ya tatu ni kutaka kuwa na wabunge bungeni watakaosaidia kubadilisha sheria kandamizi na kushinikiza upatikanaji wa Katiba mpya ambayo itaweka msingi wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikuwa na vyama vya upunzani kwa muda mrefu.
"Bunge la sasa ni la chama kimoja kamwe halitaweza kutuletea mabadiliko ya sheria...tunahitaji wabunge wapya wenye uwezo wa kuiwajibisha serikali," alisema Kigaila.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAUMA Mkoa wa Songwe, Nikubuka Kayuni, alisema chama hicho kinaendelea kuimarika ambapo hadi sasa kina wanachama 400, ikiwemo kupata ofisi ya Chama.
Katika hatua nyingine, Kigaila pia aliwatangaza rasmi na kuwakabidhi fomu wagombea wawili wa ubunge kutoka Wilaya ya Mbozi ambao ni Happiness Kwilabya anayewania jimbo la Vwawa na Michael Mwamlima kwa jimbo la Mbozi.
Mwisho.
0 Comments