NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Shule ya Msingi Good Victory imeandika historia mpya katika Mkoa wa Iringa baada ya kuibuka kinara wa shule kumi bora kwa matokeo ya Darasa la Nne, ikipata wastani wa alama 283.57 daraja A. Mafanikio haya makubwa yameifanya shule hiyo kuwa mfano wa kuigwa katika taaluma, nidhamu na usimamizi bora wa elimu.
Kwa ushindi huu, Good Victory imewazidi shule nyingi zenye historia ndefu ya kitaaluma, jambo linalothibitisha kuwa juhudi, mipango madhubuti na ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi huzaa matunda makubwa.
Walimu wa shule hiyo wamepongezwa kwa kujituma, kufundisha kwa moyo na kutumia mbinu bora za ufundishaji zinazomweka mwanafunzi katikati ya mchakato wa kujifunza.
Nafasi ya pili ilishikwa na Shule ya Msingi Sipto iliyopata wastani wa alama 277.32 daraja A, ikifuatiwa na Amini yenye 270.82, huku The Glory ikipata 269.78. Shule ya St Dominic Kigonzile ilichukua nafasi ya tano kwa alama 263.58, ikifuatiwa na Gangilongo (262.32), Asante Sana Tanzania (259.22), St Dominic Mkimbizi (256.85), St Dominic Main (256.29) na St Dominic Ngelewala iliyofunga orodha kwa alama 254.05, zote zikipata daraja A.
Hata hivyo, ushindi wa Good Victory una umuhimu wa kipekee kwani unaonesha dhamira ya dhati ya shule hiyo katika kujenga msingi imara wa elimu kwa watoto wa Kitanzania.
Mazingira bora ya kujifunzia, nidhamu ya hali ya juu na ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa shule na wazazi vimekuwa nguzo kuu za mafanikio haya.
Wazazi na wadau wa elimu mkoani Iringa wameeleza kufurahishwa na matokeo haya, wakisema Good Victory imeibua matumaini mapya kuwa elimu bora inawezekana pale ambapo kuna uwajibikaji na maono ya pamoja.
Kwa mafanikio haya, Good Victory si tu kinara wa matokeo, bali pia ni nembo ya ubora wa elimu katika Mkoa wa Iringa.







0 Comments