Na,Jusline Marco;Arusha
Shirika la RISTI Kutoka Korea Kusini kwa KUSHIRIKIANA na Wadau wa Taasisi ya Chuo cha Maji pamoja viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanya kikao cha Kutafuta suluhu ya kukabiliana na changamoto ya kiwango kikubwa cha Kemikali ya Floride kwenye Maji katika baadhi ya maeneo Mkoani Arusha.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika Julai 15, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenan Kihongosi, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Iko Tayari Kutoa ushirikiano katika hatua yoyote itakayohitajika ili kusaidia changamoto hiyo ambayo inaleta athari kubwa kwa wananchi.
Aidha amewashukuru Wadau hao kwa kuketi pamoja , na kuisaidia Serikali Kutafuta ufumbuzi ya madini hayo ambayo ni changamoto kubwa hasa katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru.
Kwa upande wake Prof. Adam Karia Mkuu wa Chuo cha Maji amesema kuwa kama ilivyo mkakati wa Serikali ya Awamu ya sita wa kuangazia afya ya wananchi na nguvu kazi Bora ili wananchi waweze kuzalisha, hiyo itakuwa ni njozi kubwa kwa wananchi kupata suluhisho la Maji Bora na salama kwa afya zao, ambapo wanaendelea na tafiti mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Seleman Msumi pamoja na kuwashukuru Wadau hao, amesema kuwa kikao hicho ni muhimu sana kwani katika Halmashauri hiyo, Kata za Oldonyosambu pamoja Oldonyowas zikiwa na takribani Vijiji vinne vimeathirika sana kutokana na madhara ya Madini ya Floride kwenye Maji wanayotumia na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.
"Tuna matumaini kuwa baada ya kikao hiki tutapata ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza kama sio kutokomeza kabisa changamoto hii kwa wananchi wetu". Amesema Msumi.
Hata hivyo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Joseph Makaidi ameeleza kuwa Mkoa huo umekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vyanzo vya uhakika vya Maji safi na salama na vingine kukumbwa na changamoto hiyo ya madini ya Floride hivyo mstakabali wa kikao hicho utasaidia kupata mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo.
0 Comments