Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeandaa warsha ya mafunzo kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa na Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika Chuo kikuu cha Dar es salaam katika ukumbi wa mikutano wa Maktaba mpya.
Warsha hiyo ilifunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Hassan Abas Rugwa. Mhe. Rugwa alisema kuwa ni jambo jema kwa Baraza kuamua kutoa elimu kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa kwani wao ndiyo wahusika wakuu katika jamii zetu.
“Natoa shukrani zangu za pekee kwa NEMC kwa ajili ya kuandaa warsha ya kutujengea uwezo sisi na watendaji wetu kama wadau muhimu katika utekelezaji wa kusimamia mazingira, kwani suala la mazingira ni suala mtambuka ambalo linahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya wadau mbalimbali katika kuyalinda mazingira yetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo” Alisema Hassan Rugwa.
Aliendelea kusema kuwa tutambue mazingira tunayotumia hivi sasa ndiyo mazingira yaliyotengenezwa na kulindwa na kizazi kilichopita hivyo kuna haja ya kuyalinda na kutengeneza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Aliongezea kuwa jamii yetu inakumbwa na changamoto mbalimbali za kimazingira kutokana na mabadiliko ya Tabianchi pamoja na ukuaji wa Nchi yetu hasa katika mambo ya maendeleo, hivyo tunatakiwa kuweka nguvu ya ziada ili tuyalinde mazingira yetu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Mhandisi Samuel Gwamaka alisema kuwa nia kubwa ya warsha hii ni kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira na kupanua uelewa kwani kero kubwa zinazotoka kwa jamii yetu ni kutokana na kutoelewa Sheria ya Mazingira na Kanuni mbalimbali zinazo ratibu utendaji.
“Katika kutafuta msingi wa kuweza kutatua changamoto na malalamiko yanayoletwa na wananchi, NEMC imeamua kutoa elimu kwa viongozi na watendaji wa Kata na Mtaa suala ambalo ndiyo suluhisho kubwa ilituweze kuweka ustawi wa mazingira katika maeneo yetu. Pia lengo letu ni kuwaelekeza majukumu yenu kisheria na kiutendaji pamoja na kuweka mahusiano ya karibu na Baraza katika kutatua changamoto za kimazingira katika jamii yetu” Alisema Dkt. Gwamaka.
Dkt. Gwamaka alimaliza kwa kusema kuwa mwisho wa warsha hii kila mtu atatambua majukumu yake katika kusimamia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014, Kanuni na Miongozo ili kuwafanyia watanzania kazi ambayo wametutuma tuwatumikie kwa weledi na waweze kuishi maisha yao katika mazingira yaliyo safi na salama.
Naye Mtendaji wa Kata ya Mbweni Bi. Zuhura Almas aliipongeza NEMC kwa elimu waliyoipata kwani kwake itakuwa chachu ya kuwa balozi mzuri wa kusimamia utunzaji wa mazingira katika eneo lake kwa ajili ya kukinusuru kizazi kilichopo na kijacho.
0 Comments