Header Ads Widget

RAIS SAMIA AZINDUA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050, ATOA WITO WA MABADILIKO YA FIKRA KWA WATANZANIA

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 jijini Dodoma, akisisitiza kuwa nyaraka hiyo inalenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa juu, unaojitegemea, jumuishi na endelevu.


Akizungumza katika hafla hiyo ya kihistoria Julai 17,2025 Jijini Dodoma , Rais Samia amesema kuwa Dira hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia maoni ya makundi yote ya kijamii, bila kupoteza mila, desturi na maadili ya Kitanzania ambayo ni msingi wa utambulisho wa taifa.


 “Dira hii si ya watu wachache; ni ya Watanzania wote. Imechukua maoni ya kila kundi vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, sekta binafsi, wazee, na hata Watanzania wanaoishi nje ya nchi,” alisema Rais Samia.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira hiyo yanahitaji mabadiliko ya fikra na mitazamo, kuanzia Serikali Kuu, mamlaka za mitaa, sekta binafsi hadi kwa wananchi kwa ujumla, ili kila mmoja awe sehemu ya suluhisho badala ya kuwa mtazamaji.


Aidha, Rais Samia alieleza kuwa Dira ya 2050 inalenga kuijenga Tanzania yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi, kwa kupunguza utegemezi wa mikopo mikubwa ya nje, huku ikitoa kipaumbele kwa uendelezaji wa rasilimali watu, hususan vijana.

 “Tumeshuhudia katika nchi zilizoendelea, idadi ya wazee imezidi ile ya vijana. Lakini Tanzania ina rasilimali kubwa ya vijana  ambao katika mchakato wa Dira hii wamekuwa mstari wa mbele kutoa maoni yao,” aliongeza Rais Samia.

Dira ya Maendeleo ya 2050 inakuja kukamilisha Dira ya Maendeleo ya 2025, ambayo imekuwa mwongozo wa taifa kwa zaidi ya miongo miwili. Dira mpya inatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi kuanzia Julai 2026.


Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa dira hiyo ni muhimu kwani hakuna taifa linalopata maendeleo kwa kubahatisha.

“Maendeleo hayaji kwa bahati mbaya. Yanahitaji mipango madhubuti. Dira hii ni mwanzo mzuri kuelekea miaka ijayo yenye matumaini,” amesema Dkt. Mpango.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza uandaaji wa dira hiyo akisema inajikita kwenye mahitaji ya watu, hasa kupitia uwekezaji katika rasilimali watu, usimamizi wa mazingira na usawa wa kijinsia.

Katibu Mtendaji mkuu Mipango na uwekezaji wa tume ya taifa ya mipango Dkt Fred Msemwa akieleza kuhusu mchkato wa maandalizi wa dira 2050


 amesema kuwa mchakato huo umechukua takribani miaka miwili na umehusisha ushirikishwaji mpana wa wananchi, ambapo Watanzania milioni 1.174 walitoa maoni yao kwa njia mbalimbali. 

Aidha, zaidi ya wananchi 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa na kutoa maoni yao kuhusu mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

"Tulifanya utafiti wa kina kwa nchi zilizopiga hatua na kufikia uchumi wa kati, kwa lengo la kujifunza na kutumia maarifa yao kufanikisha maendeleo tunayoyataka. Malengo ya Tanzania ni kufikia uchumi wa kati kwa njia endelevu,"amesema Msemwa.


Ameeleza kuwa Rasimu ya Dira ya 2050 ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki ili kuhakikisha maoni yao yamezingatiwa kikamilifu. Baada ya hatua hiyo, nyaraka hiyo iliwasilishwa katika makundi mbalimbali ya kijamii, kitaaluma na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa hakuna jambo muhimu lililosahaulika.

Msemwa ameongeza kuwa Dira hiyo mpya ya Maendeleo itaanza kutekelezwa rasmi mwezi Julai 2026, mara baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Amesema Dira hiyo Mpya imetumia muda na fedha nyingi ili kukamilika kwake

Akieleza kuhusu maudhui ya Dira 2050 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa dira hiyo imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, na iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Juni mwaka huu.

 “Hii ni dira shirikishi, inayolenga kuweka misingi ya maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Imelenga pia kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa ushindani na viwanda unaotoa ajira na kukuza ubunifu,” ameeleza.


Aidha ameitaja misingi Mikuu ya Dira ya 2050 kuwa ni pamoja na Demokrasia, Haki na Uhuru,Utu, Amani na Umoja wa Kitaifa,Utajiri na Matumizi Endelevu ya Rasilimali Asilia,Utamaduni na Maadili ya Kitaifa na Uchumi wa Kisasa unaojumuisha wote. 

Amefafanua kuwa Dira hiyo imeweka vipaumbele kwenye sekta za elimu, afya, teknolojia, kilimo cha kisasa, mabadiliko ya tabianchi, miundombinu na ushirikishwaji wa wanawake na vijana.


Akitoa salamu za sekt binafsi Rostam Azizi amesema Ili tanzania ipige hatua kubw hakuna budi kuwekeza kwenye rasilimali watu ambao ni vijana. 

Lakini aliomba vyuo vyandani kuimalisha na kuboresha mitaala ili kutoa vijana watakao kubalika katika soko la ndani na lakimataifa


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI