Waandishi wa habari kutoka mikoa ya kanda ya Magharibi wakiwa katika kikao kazi na maafisa na watendaji wa TMDA mkoani Tabora
Na Fadhili Abdallah,Tabora
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) Dk.Adam Fimbo amesema kuwa hakuna dawa za kuongeza ukubwa wa makalio wala matiti ambayo imeidhinishwa na mamlaka hiyo nchini hivyo wote wanaotangaza kutengeneza na kuuza dawa hizo ni feki.
Dk.Fimbo ametoa maelezo hayo akizungumza kwenye kikao kazi cha TMDA na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya kanda ya magharibi kutoka mikoa ya Kigoma,Tabora na Katavi ambapo amebainisha kuwa hakuna dawa hizo zilizothibitishwa na mamlaka yeyote hapa nchini.
Mkurugenzi huyo wa TMDA amewataka Watanzania wasihadaike na matangazo au watu wanaotangaza kuuza dawa za kuongeza makalio, matiti na maeneo mengine ya mwili wa binadamu wanaofanya hivyo ni kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kutokana na hilo ametaka wananchi na kama kuna mahali yupo mtu ameweka duka au sehemu anayoeleza kuuza dawa hizo watoe taarifa TMDA wachukue hatua kwa watu hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Dawa kutoka TMDA,Dk.Kissa Mwita alisema kuwa mamlaka hiyo inayo mifumo madhubuti inayosimamia katika kuhakikisha dawa zinazotumika hapa nchini zimepata idhini ya mamlaka za serikali ikiwemo TMDA ili kuzuia matumizi holela ya dawa au dawa zisizofaa ambazo zinaweza kuleta madhara kwa binadamu.
Mwisho.
0 Comments