Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanzisha mkakati kabambe wa kuendeleza maeneo ya Fumba kuwa mji maalum wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha maendeleo ya kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkakati huu unalenga kuhimiza ubunifu wa kiteknolojia, kuvutia wawekezaji wa kimataifa na kuwajengea vijana mazingira rafiki ya kujiajiri kupitia teknolojia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo juu ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasilino la Zanzibar (ZICTIA) Mhandisi Shukuru Awadhi Suleiman amesema kuwa, Mji wa Tehama utakuwa na miundombinu ya Kisasa kama vile nyumba za makazi za kisasa, Maduka, kituo cha Data (Data Centre), Maabara bunifu (Innovation Labs) pamoja na vituo vya mafunzo kwa vijana.
Amesema kuwa, Mpango mkakati huo unalenga unalenga kuwapa fursa wataalamu wa ndani na wa kimataifa kushirikiana katika suluhisho za kidijitali zitakazosaidia kuchochea uchumi wa Zanzibar.
“Hata hivyo tunataka tupafanye kuwa ni makao mkuu ya Makampuni makubwa ya mtandao ya Dunia katika ukanda wa Afrika mashariki kwa mfano, kampuni ya Microsoft, Facebook na Google,” amesema.
“Tunaendelea kujenga mazingira rafiki ili iwe rahisi kuyashawishi makampuni hayo kuja Tanzania kuwekeza,” ameongeza.
Ameleza, Serikali tayari imeanza mchakato wa kutafuta wawekezaji na wadau wa maendeleo kushirikiana katika utekelezaji wa mradi huo.
Aidha ameeleza, sheria na miongozo ya kuendeleza mji huo zipo mbioni kukamilishwa ili kuhakikisha mazingira bora ya biashara na uvumbuzi.
Eneo la Fumba limechaguliwa kutokana na miundombinu yake inayopanuka kwa kasi na ukaribu wake na jiji la Zanzibar.
00000
0 Comments