Header Ads Widget

MAVUNDE AKABIDHI SIMU JANJA KWA WENYEVITI 222 DODOMA KUTAMATISHA RASMI UBUNGE WAKE.

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

MBUNGE wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametangaza rasmi kutamatisha kipindi chake cha miaka 10 cha ubunge, huku akikabidhi rasmi vifaa vya kidigitali Simu Janja  (Smartphone) kwa wenyeviti wote wa mitaa ili kuimarisha usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi.



Akizungumza wakati wa hafla hiyo jijini Dodoma, Mavunde amesema kuwa simu hizo zimeunganishwa na mfumo maalum wa kiteknolojia unaowezesha viongozi wa mitaa kuripoti changamoto moja kwa moja kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kwa Mbunge, hatua inayolenga kurahisisha upokeaji na majibu ya haraka kwa matatizo ya wananchi.


"Kupitia mfumo huu, kero yoyote kutoka kata yoyote inaweza kufikishwa ndani ya dakika moja kwa viongozi husika. Ni mfumo wa kwanza wa aina yake hapa Dodoma, na naamini utaboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wananchi," alisema Mavunde.


Ameeleza kuwa lengo lake tangu alipoingia madarakani halikuwa kuwa kiongozi wa amri, bali mtumishi wa wananchi, akisisitiza kuwa utumishi wa umma ni wito wa kuwahudumia watu na si nafasi ya madaraka.


Katika hotuba yake, Mavunde aligusia baadhi ya matukio yaliyomgusa kibinafsi katika utumishi wake, yakiwemo ya wananchi waliokuja kuomba msaada wa kusafirisha miili ya marehemu na tukio la mtu kumbeba ndugu yake aliyefariki kwa baiskeli. 


Alisema tukio hilo lilimshawishi kununua gari kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii, licha ya kukosolewa na baadhi ya watu.


"Nilinunua gari kwa ajili ya kusaidia wananchi. Ingawa nilitukanwa na kubezwa kuwa sina maono, gari hilo limekuwa msaada mkubwa kwa jamii," alieleza.


Mavunde amesema simu janja  hizo  hazitakuwa kwa matumizi ya anasa bali ni nyenzo za kushughulikia matatizo ya wananchi na hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa awali.


Mbali na kugawa vifaa hivyo, Mavunde alichangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa sare za kazi (sakosi) kwa wenyeviti, akisisitiza kuwa anamaliza kipindi chake cha ubunge akiwa ametimiza dhamira ya kuwahudumia wananchi.


"Kesho, Juni 27, 2025, ninamaliza rasmi kipindi changu kama Mbunge wa Dodoma Mjini. Nafurahi kusema kuwa nimejitahidi kutimiza ahadi zangu. Kama kuna mambo sijaweza kuyakamilisha, nitaomba kushirikiana na atakayekuwa mbunge mpya ili tuendelee kuyafanikisha kwa pamoja," alisema.


Kwa upande wake, Charles  Mamba  Mwenyekiti CCM wilaya ya Dodoma Mjini , aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha siasa za kubahatisha na kujiandaa kwa uchaguzi ujao kwa umakini. Alisisitiza kuwa kutoa ni moyo na si lazima iwe sehemu ya ahadi ya kisiasa.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI