Beatus Nchota Meneja wa TRA mkoa Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoa Kigoma imekamata na kuteketeza bidhaa mbalimbali za vyakula na vipodozi tani 53 zenye thamani ya shilingi milioni 530 ambazo ziliingizwa nchini bila kufuata taratibu.
Meneja wa TRA mkoa Kigoma, Beatus Nchota akitoa taarifa kwa waandishi wa habari wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo katika dampo la kuputia uchafu lililopo Buhanda Businde Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.
Kiongozi huyo alisema kuwa bidhaa hizo ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu zilikamatwa kwa kipindi cha miaka miwili katika operesheni mbalimbali zilizofanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama Zikiwa hazina vibali vya mamlaka mbalimbali kuruhusiwa kuingizwa nchini.
Bidhaa zilizokamatwa zimetajwa kuwa ni pamoja na vipodozi haramu aina ya Pawpaw cream, Cocopulp, Epidem, vinywaji vya kusisimua mwili vikiwemo Akayabagu na Eloko ya Mibali, Pombe kali aina ya Warag, Amstel, Pendo Gin,Hozagara na Akanovera, sigara hatari aina ya Bharat na Super Mathc zikiwemo pia nyavu zilizopigwa marufuku, dawa za binadamu na sikari.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Magharibi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), Christopher Lugoa alisema kuwa ameshiriki kwenye utekelezaji wa shehena hiyo kutokana na Mamlaka za kisheria kuipa TMDA mamlaka ya kuthibitisha kwamba bidhaa za vyakula na dawa vilivyokamatwa kwa wakati huo hazifai kwa matumizi ya binadamu ambapo wamefanya ukaguzi na kuthibitisha kwamba bidhaa hizo hazifai kwa matumizi.
Naye Afisa Udhibiti ubora wa bidhaa wa Shirika la Viwango (TBS) kanda ya magharibi, Ezekiel Mobuti alisema kuwa sheria imewapa mamlaka ya kusimamia viwango mbalimbali vya kitaifa na kimataifa vilivyowekwa na kwamba bidhaa ambazo hazijafikia viwango vinapaswa kutekekezwa kama ambavyo katika bidhaa zilizokamatwa zipo ambazo hazijapata vibali vya TBS kwa ajili ya kutumika nchini.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Kigoma Monea Juma na Rashidi Jumanne ambao walishuhudia uteketezaji huo wameipongeza TRA na taasisi nyingine za serikali kwa kufanya jambo ambapo wameeleza kuwa bidhaa hizo zikiingia mtaani ni hatari kwa afya za binadamu.
0 Comments