Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo leo juni 10,2025 ameanza ziara ya siku 4 Kata kwa Kata kusoma utekelezaji wa ilani huku wanachama wakimchangia fedha kuchukua fomu.
Kishindo cha mbunge huyo kimeanzia Kata ya Rwamlimi,Bweri,Kitaji na kunalizia Nyakato ambako kote amepata mapokezi makubwa.
Akiwa kituo cha kwanza Kata ya Rwamlimi wajumbe wa Mkutano Mkuu waliohudhuria kikao hicho wameguswa na utendaji kazi na utekelezaji wa ilani uliofanywa na mbunge huyo na kuamua kumchangia fedha za kuchukua fomu kugombea tena nafasi hiyo.
Wakizungumza na Matukio Daima wanachama hao wamesema yaliyofanywa na mbunge huyo chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho hawana budi kumuunga mkono tena.
Wamesema kwenye sekta moja tu ya elimu ni mambo makubwa yamefanyika lakini kwa mbunge hadi sasa anaendelea na utengenezaji wa madawati,viti na meza kwaajili ya shule za msingi na sekondari na tayari vifaa hivyo vimeshafikishwa mashuleni.
Wajumbe hao wamesema hakuna mwananchi aliyechangishwa fedha kwenye utengenezaji wa madawati na viti hivyo bali ni fedha za mfukoni za mbunge huyo hivyo watamlipa kwa kumchagua tena.
Diwani wa Kata ya Rwamlimi Kurwa Paulo Mahamba amesema hawawezi kufanya makosa na watakwenda na mbunge huyo kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa amefanya makubwa.
Kwenye muendelezo wa zìara ya leo mbunge huyo amechangiwa fedha za kuchukua fomu kwenye Kata za Bweri,Kitaji na Nyakato kwa kutekeleza vyema ilani.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Kata hizo mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amewashukuru wanachama wa CCM na wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Kata hizo kwa kumpa ushirikuano kwa miako 5.
Amesema kutokana na ushirikiano alioupata ndio uliomfanya kutekeleza ilani kwa kipindi cha miaka 5 kwa kusukuma miradi ya maendeleo.
" Nimeona kwa kipindi hiki kilichobaki niombe ruhusa kuja kuwashukuru kwa namna mlivyonipa ushirikiano kwa kipindi cha miaka 5.
" Niwashukuru kwa michango yenu kwaajili ya kuchukua fomu na niwaahidi nipo tayari kuwatumikia kwa kipindi kingine kwa kuwa bado ninazo nguvu za kuwatumikia",amesema.
Mbunge huyo amesema wanaosema porojo wapuuzwe waangalie maendeleo yaliyofanyika ndani ya jimbo la Musoma mjini na kudai makubwa zaidi yatafanyika.
Kesho ziara hiyo ya usomaji utekelezaji wa ilani utaendelea kusomwa kwenye Kata za Mshikamano,Buhare,Iringo na Kigera.
0 Comments