Na Matukio Daima App.
TABORA.Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Lufigo Bundala, mkazi wa Kijiji cha Ibuta kilichopo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuanzisha vurugu, kushambulia na kujeruhi watu katika mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliofanyika leo Jumanne Juni 10, 2025.
Akizungumza na viongozi wa Chadema waliofika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Igunga, Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Meshack Sumuni amesema polisi inawasaka vijana wawili kuhusiana na tuhuma hizo.
Bundala pamoja na wenzake waliofanikiwa kukimbia wanatuhumiwa kuanzisha vurugu kwa kupiga kelele, kurusha mawe na kujeruhi watu wakati wa mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Igunga.
"Kwanza, Jeshi la Polisi tunatoa pole na tunasikitishwa kwa kilichotokea; na tayari tunamshikilia mtu mmoja na tunawasaka wengine wawili kwa mahojiano," amesema Sumumi.
Kutokana na tukio hilo, OCD Sumuni amesema jeshi hilo tayari imeimarisha ulinzi katika mikutano mengine ya Chadema itakayofanyika wilayani Igunga.
Hata hivyo, maelezo hayo ya OCD Sumuni hayakuwaridhisha viongozi wa Chadema ambapo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amehoji kwanini askari polisi hawakuwepo eneo la mkutano wakati wa vurugu.
Akijibu swali hilo, OCD Sumuni amesema ofisi yake iliwatanguliza askari kanzu ambao ndio walifanikiwa kuwanasa kumkamata mmoja wao na kutiwa mbaroni.
Akizungumzia tukio hilo akiwa ofisini kwa OCD, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema chama hicho kilipata taarifa za uwepo wa njama za kuvuruga mkutano wa Igunga na ilitimiza wajibu kwa kuzifikisha polisi, hivyo wanasikitika kitendo cha Jeshi la Polisi kutochukua hatua madhubuti hadi watu wamejeruhiwa.
0 Comments