![]() |
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
KIONGOZI Mstaafu wa Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amechukua fomu ndani ya chama chake akionesha nia ya kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini katika uchaguzi Mkuu ujao.
Kabwe akichukua fomu katika ofisi za ACT Wazalendo jimbo la Kigoma Mjini akisindikizwa na idadi kubwa ya viongozi wa chama hicho katika matembezi yaliyoanzia ofisi za ACT Wazalendo mkoa Kigoma zilizopo Ujiji.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Jimbo Zitto alisema kuwa ameamua kurudi kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini baada ya kuona hali ya maendeleo ya jimbo hilo ikiwa siyo nzuri miaka mitano baada ya kuwa yuko nje ya ubunge katika jimbo hilo.
Kiongozi huyo alisema kuwa pamoja na nia yake ya kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini alisema kuwa uchaguzi huu hautakuwa rahisi kama ambavyo ilitokea mwaka 2020 hivyo kuwataka wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanazisimamia kura zao kikamilifu.
Zitto alisema kuwa anamuomba Raisi Samia Suluhu Hassan kuruhusu uchaguzi kuwa huru na haki ili Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi Imtangaze mgombea atakayechaguliwa na wananchi.
Zitto alikabidhiwa fomu ya kugombea katika uchaguzi wa ndani wa chama na Katibu wa ACT jimbo la Kigoma Mjini, Iddi Adam ambaye amewataka wanachama wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu katika zoezi litakalofungwa Mei 28 mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa Kigoma, Kiza Mayeye amechukua fomu kugombea ubunge katika jimbo la Kigoma Kaskazini wilaya ya Kigoma akisema kuwa uchaguzi huu ni muhimu kwa chama Chao kurejesha Bungeni wabunge wake ili kusimamia maslahi ya wananchi.
Mayeye alisema kuwa tangu mwaka 2020 wabunge waliopo wamepoteza mwelekeo kwa kuangalia maslahi yao na kuacha kusimamia maslahi ya wananchi wanaowaongoza.
Mwisho.

0 Comments