Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SERIKALI imeanza kushughulikia changamoto ya mvua kwa wakazi wa eneo la Katubuka ambao nyumba zimezingirwa na maji manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma baada ya Idara ya Maafa ya ofisi ya Waziri Mkuu kukabidhi kwa Mkuu wa mkoa Kigoma misaada mbalimbali kwa ajili ya waathirika hao ikiwemo misaada ya chakula ili na vifaa vya matumizi ya nyumbani ili kukabiliana na changamoto iliyowatokea.
Kaimu Mkurugenzi idara ya Maafa ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Celestine Masamalago alikabidhi misaada hiyo mkoani Kigoma huku akieleza kuwa mpango huo unatekeleza baada ya ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma kuomba ofisi ya Waziri Mkuu kupatiwa misaada hiyo.
Masamalago aliitaja misaada ya kibinadamu iliyotolewa kuwa ni tani 15.6 za mahindi, tani 4.6 za maharage, magodoro, 283, Blanket 283, Ndoo 283 na mikeka 283 ambapo misaada hiyo itatolewa kwa kaya 283 zenye jumla ya watu 1304 na kwamba itatosheleza kwa mwezi mmoja.
Akizungumzia baada ya kupoea misaada hiyo ya kibinadamu Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye ameishukuru serikali ya Raisi Samia kwa kuona na kujali madhira yaliyowapata wananchi hao wa eneo la Katubuka,Kibirizi na Bangwe manispaa ya Kigoma Ujiji na kwamba hiyo ni hatua ya awali katika kushughulikia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo na kwamba serikali imeshatuma wataalam kufanya tathmini ili kuchukua hatua kurekebisha eneo hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Kigoma,Rshidi Chuachua akizungumza baada ya kukabidhiwa misaada hiyo na Mkuu wa mkoa Kigoma, alisema kuwa ameipongeza serikali ya Rais Samia kwa kuona umuhimu wa jambo hilo lililowatokea wananchi wa Katubuka sambamba na Bunge la Tanzania kutoa muda kwa mbunge wa jimbo la Kigoma, Kilumbe Ng’enda kutoa hoja ya kuiomba serikali kusaidia jambo hilo.
Aidha kwa niaba ya wananchi wa manispaa ya Kigoma Ujiji waliokumbwa na madhira hayo Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda ameishukuru serikali kupitia idara ya maafa ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa msaada huo wa kibinadamu kujibu maombi ya misaada ya wananchi hao na tayari timu ya kufanya tathmini ya madhara yaliyotokea eneo hilo imefika na kutembelea eneo hilo na kuzungumza na watu mbalimbali ikiwa ni baada ya hoja iliyotolewa bungeni kuomba bungeni kujadili kwa dharula maafa yaliyotokea eneo hilo.
Mwisho.
0 Comments