Header Ads Widget

CCM YATANGAZA MAJINA YA WAGOMBEA UBUNGE 2025 BAADHI YA VINARA WA KURA ZA MAONI WAACHWA

 



Na Hamida Ramadhan, Dodoma


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza orodha ya makada waliopitishwa kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 baada ya mchujo uliofanywa na vikao vya juu  vya chama hicho. 


Wakati baadhi ya majina yakiendelea na safari ya kisiasa, waliokuwa vinara kwenye kura za maoni wamejikuta wakiondolewa katika hatua za mwisho.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA  Amos Makalla amesema uteuzi huo umefanywa na vikao vya maamuzi vilivyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.


Makalla amesema baadhi ya waliokuwa wakiongoza kwenye kura za maoni lakini majina yao hayakurudishwa ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Tanga Mjini Ummy Mwalimu na Samuel Malecela ambaye aliongoza kura za maoni katika Jimbo la Dodoma Mjini.


Katika Jimbo la Kigoma Mjini, chama kimempitisha Clinton Revocutus maarufu kama Baba Leo licha ya kutoshinda katika kura za maoni. 


Hata hivy hali kama hiyo imetokea katika majimbo mengine ambapo baadhi ya waliokuwa wa pili au wa tatu kwenye kura za maoni wamepitishwa kuwa wagombea wa chama.


Majina mengine yaliyopenya licha ya kutoshinda kura za maoni ni Ester Matiko katika Jimbo la Tarime Mjini, Ester Bulaya Bunda Mjini, Magreth Sitta Urambo na Exaud Kigahe aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.


Wagombea wengine waliopitishwa na chama ni Paul Makonda katika Jimbo la Arusha Mjini, Nape Nnauye Mtama, Kangi Lugola Mwibala, Livingston Lusinde Mvumi na Isaya Moses ambaye anachukua nafasi ya aliyekuwa Spika wa Bunge Hayati Job Ndugai katika Jimbo la Kongwa.


Katika hatua nyingine Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imemteua Balozi Dk Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wa CCM akichukua nafasi ya Balozi Dk Emmanuel Nchimbi ambaye sasa ni mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya chama hicho.


Aidha Kenani Kihongosi ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Amos Makalla ambaye amesema huu ndio ulikuwa mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari katika nafasi hiyo na kuwaomba wampe ushirikiano mrithi wake.


Viongozi wengine walioteuliwa ni pamoja na Joshua Milumbe ambaye sasa ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI