Rais wa Marekani Donald Trump amesema "hajafurahishwa" na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, kufuatia shambulio kubwa zaidi la anga dhidi ya Ukraine.
Katika hali ambao ni nadra sana kutokea, Trump alisema: "Ni kitu gani kilichomtokea? Anaua watu wengi sana." Baadaye alimwita Putin "mwendawazimu".
Awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema "ukimya" wa Marekani juu ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi ndio unaompa kiburi Putin, akitoa "shinikizo" - ikiwa ni pamoja na vikwazo vikali - dhidi ya Urusi.
Takriban watu 12 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Ukraine usiku wa kuamkia Jumapili baada ya Urusi kufanya shambulizi la ndege zisizo na rubani na makombora 367 - idadi kubwa zaidi katika usiku mmoja tangu Putin alipoanzisha uvamizi nchini humo mnamo 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini New Jersey siku ya Jumapili, Trump alisema: "Nimemfahamu Putin kwa muda mrefu, nilishirikiana naye kila wakati, lakini anatuma makombora mijini na kuua watu, na sifurahii hata kidogo."
Alipoulizwa iwapo anafikiria kuongeza vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi, Trump alijibu: "Kabisa." Rais wa Marekani ametishia mara kwa mara kufanya hivyo kabla - lakini bado hajaweka vikwazo vyovyote dhidi ya Moscow.
Muda mfupi baadaye, Trump aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social kwamba Putin "amekuwa mwendawazimu kabisa".
"Nimekuwa nikisema kwamba anataka Ukraine yote, sio kipande tu, na labda hiyo inathibitisha kuwa kweli, lakini ikiwa atafanya hivyo, itasababisha kuanguka kwa Urusi!"
Lakini Trump hakumsaza hata Zelensky, alimtolea maneno makali na kusema kuwa "haifanyii nchi yake vizuri kwa jinsi anavyozungumza".
"Kila kitu kutoka kinywani mwake kinasababisha matatizo, sifurahii, na itakuwa bora ikiwa ataacha" Trump aliandika kuhusu Zelensky.
0 Comments