Takriban Wapalestina 24 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya anga ya Israel usiku kucha, ikiwa ni pamoja na shambulizi dhidi ya shule ambayo ni makazi kwa familia zilizohamishwa katikati mwa Gaza, kulingana na madaktari na maafisa wa ulinzi wa raia.
Shambulizi hilo lililenga shule ya Fahmi Al-Jargawi katika Jiji la Gaza, ambayo imekuwa ikihifadhi mamia ya watu waliokimbia makazi yao kaskazini wa Beit Lahia, ambao kwa sasa unashuhudia mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la Israel.
Msemaji wa shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza linaloendeshwa na Hamas alisema miili 20, ikiwa ni pamoja na watoto, iliokolewa shuleni humo - wengi wao wakiwa wameungua vibaya - baada ya moto kuteketeza vyumba viwili vya madarasa.
Wanajeshi wa Israel wametafutwa ili kutoa maoni yao.
"Moto ulikuwa kila mahali. Niliona miili iliyoungua ikiwa imelala chini," alisema Rami Rafiq, mkazi anayeishi mkabala na shule hiyo, kupitia simu na BBC. "Mwanangu alizimia alipoona tukio hilo la kutisha."
Kanda za video zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha moto mkubwa ukiteketeza sehemu za shule, zikiwa na picha za waathiriwa walioungua vibaya, wakiwemo watoto, na walionusurika wakiuguza majeraha mabaya.
Ripoti za ndani zilisema miongoni mwa waliofariki ni Mohammad Al-Kasih, mkuu wa uchunguzi wa polisi wa Hamas kaskazini mwa Gaza, pamoja na mke wake na watoto.
Muda mfupi kabla ya shambulizi la shule, shambulio lingine la anga la Israeli lilishuhudiwa katika nyumba moja iliyopo katikati mwa jiji la Gaza, na kuua watu wanne zaidi, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas ilisema.
Mashambulizi hayo mawili ni sehemu ya mashambulizi makubwa ya Israel ambayo yameongezeka katika sehemu ya kaskazini ya eneo hilo kwa muda wa wiki moja iliyopita.
0 Comments