Na Matokeo Daima App.
DODOMA.Serikali imesema haitowavumilia wageni haramu wanaoingia nchini kwa nia ya kuhatarisha amani, na imeeleza kuwa watu wa aina hiyo ni wahalifu watakaoshughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 26, 2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri Bashungwa amesema kuwa, licha ya jitihada endelevu za serikali kuvutia wageni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo, hakutakuwa na muhali kwa wageni wachache wenye nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi.
"Wageni waovu hawana nafasi nchini. Serikali haitowavumilia wageni wanaoingia kwa lengo la kuhatarisha usalama na amani ya nchi yetu. Naipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kwa udhibiti wa wageni haramu na wale wanaokiuka masharti ya vibali vyao," amesema Waziri Bashungwa.
Ameongeza kuwa wageni wanaoingia nchini kwa kibali maalum lakini wakajihusisha na shughuli kinyume na masharti ya vibali hivyo, wanachukuliwa kama wahalifu kama walivyo wahalifu wengine, na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa sheria za nchi.
0 Comments