Header Ads Widget

MAHUSIANO MAZURI NI NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU-MHE.SAGINI*


Mahusiano mazuri kazini yameelezwa kuwa msingi muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali katika ngazi mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo Mei 26, 2025 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini, alipokuwa akitoa mada kuhusu Muundo wa Serikali, Taratibu za Utendaji kazi Serikalini na Mawasiliano ndani ya Serikali kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wanaoshiriki mafunzo ya uongozi yanayoendelea Kibaha, mkoani Pwani.

Mhe. Sagini amesema kuwa mahusiano mazuri ya kikazi baina ya viongozi, watumishi na wadau wengine ni msingi wa usimamizi bora wa rasilimali watu na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

“Ni muhimu sana kuwa na mahusiano chanya kazini, kwa sababu nyinyi ndiyo kiungo kati ya Serikali Kuu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Uhusiano mzuri huleta mshikamano, hurahisisha utekelezaji wa sera, na huongeza ari ya kazi miongoni mwa watumishi,” amesema Mhe. Sagini.

Ameongeza kuwa uongozi wa kisasa unahitaji viongozi waliobobea si tu katika usimamizi wa kazi, bali pia katika kujenga mazingira rafiki ya kazi, yanayozingatia mawasiliano mazuri, heshima na ushirikiano wa karibu.

Mafunzo hayo ambayo yanaendelea kwa siku kadhaa yanalenga kuwaongezea viongozi hao maarifa na mbinu bora za uongozi, ili waweze kusimamia kwa weledi sekta wanazoziongoza, huku wakikuza maendeleo ya kiuchumi, biashara na uwekezaji katika mikoa yao.

 Kwa mujibu wa mafunzo hayo, mada mbalimbali zinazotolewa zitawawezesha washiriki kuboresha mbinu za utendaji, kuongeza tija mahala pa kazi, na kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kufanikisha malengo ya Serikali.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI