.
Safari yake ya maisha kabla ya kuwa kiongozi mpya wa kiroho wa Wakatoliki duniani na Mkuu wa nchi ya Vatican.
Na Matukio Daima Medi
Katika historia ndefu ya uongozo wa Kanisa Katoliki, kila kizazi huja na kiongozi anayebeba matumaini, changamoto na dira mpya.
Mei 8 2025, Kanisa hilo lilimshuhudia Robert Francis Prevost, mzaliwa wa Chicago, Marekani, akichaguliwa kuwa Papa wa 267 na kuchukua jina la Leo wa XIV.
Huyu ndiye Papa Leo wa XIV —kiongozi mpya wa kiroho wa Wakatoliki 1.4 bilioni kote duniani, na mtawala wa jiji na nchi takatifu ya Vatican.
Lakini kabla ya kuwa kiongozi wa kiroho mwenye ushawishi mkubwa duniani, Prevost (Papa Leo wa XIV) alikuwa na maisha ya kawaida, yaliyosheheni huduma, kujifunza, na kujitoa kwa ajili ya wito wa kipadri.
MWANZO WA SAFARI YAKE.
Papa Leo wa XIV alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955 huko Illinois katika jiji la Chicago, chini Marekani.
Ni mtoto wa tatu wa familia ya Louis Marius Prevost, mwanajeshi wa zamani wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani, na Mildred Martinez, akiwa na asili ya Kifaransa, Kiitaliano na Kihispania, Prevost alikua katika mazingira ya tamaduni mchanganyiko yaliyomjengea maono mapana ya huduma ya kibinadamu.
Alihitimu sekondari katika seminari ya Shirika la Mtakatifu Augustine mwaka 1973, na baadaye kusomea Sayansi ya Hisabati katika Chuo Kikuu cha Villanova.
Lakini badala ya kufuata kazi ya taaluma hiyo, aliitikia wito wa maisha ya kitume, akiingia rasmi shirika hilo mnamo mwaka 1977.
Kutoka Marekani hadi nchini Peru na Huduma ya Umisionari.
Prevost alionyesha moyo wa utumishi wa kweli alipojitolea kwenda Peru kama mmisionari mwaka 1985.
Katika kipindi hicho, aliwahi kuwa paroko, afisa wa dayosisi, na mwalimu wa seminari, zaidi ya hapo, alikuwa msimamizi na hakimu wa mahakama ya kanisa ya kikanda.
Mwaka 1998, aliitwa kurudi Marekani kuwa mkuu wa mkoa wa Waaugustino huko Chicago. Mwaka 2001, alichaguliwa kuwa Mkuu wa Kimataifa wa Shirika la Waaugustino, akihudumu kwa mihula miwili hadi mwaka 2013.
Huu ulikuwa uongozi wa juu uliompa uzoefu mpana katika masuala ya kanisa duniani.
KIONGOZI WA KANISA NCHINU PERU.
Baada ya kipindi kifupi cha utumishi Chicago, Prevost aliteuliwa kuwa Askofu wa Chiclayo, nchini Peru mwaka 2014. Katika nafasi hii, alijenga urafiki wa karibu na waumini, aliimarisha elimu ya kikristo na kuongoza miradi ya kijamii.
Alijizolea heshima kubwa, si tu kama kiongozi wa kiroho bali pia kama mtetezi wa masikini.
Kipindi chake nchini Peru kilimuwezesha kuwa na uraia wa nchi hiyo pamoja na ule wa Marekani – ishara ya moyo wake wa kuwa sehemu ya jamii anazozitumikia.
SAFARI YA KUPANDA MADARAJA KATIKA KANISA.
Katika mwaka wa 2023, Papa Francis alimteua Prevost kuwa mkuu wa Idara ya Maaskofu (Dicastery for Bishops), mojawapo ya nafasi nyeti ndani ya Vatican.
Alisimamia uteuzi wa maaskofu kote duniani na kuchukua usukani wa mwelekeo wa uongozi wa Kanisa.
Tarehe 6 Februari 2025, Prevost alipewa hadhi ya kuwa kardinali askofu, hatua iliyomuweka katika mstari wa mbele kuwa mmoja wa wagombea wa upapa pindi nafasi hiyo ilipokuwa wazi.
PAPA LEO WA XIV NA MWANZO MPYA.
Katika siku ya pili ya kikao cha uchaguzi wa Papa (Conclave), makardinali walimchagua Prevost kuwa Papa mpya.
Kwa kuchukua jina Leo wa XIV, alijiunga na mstari wa Mapapa waliotangulia wenye jina hilo, akimfuata Papa Leo wa XIII, aliyekuwa maarufu kwa juhudi zake za kijamii karne ya 19.
Anakuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika Kaskazini, na pia wa kwanza kutoka Shirika la Waaugustino tangu karne ya 15.
Kuchaguliwa kwa Papa Leo kunaashiria mwelekeo mpya wa Kanisa katika karne ya 21 – mwelekeo unaothamini utume wa kimataifa, uzoefu wa kijamii, na ari ya kuunganisha mataifa kupitia imani.
Mwisho.
0 Comments