Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WADAU wa Pamba wameipongeza serikali kwa kuanzisha Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), jambo ambalo limeleta nidhamu katika sekta ya Pamba ikiwemo kudhibiti ubora, kuongeza uzalishaji, kupata takwimu sahihi za Pamba na wakulima.
Aidha, wadau hao pia wameipongeza Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Pamba kwa kuanza maandalizi mapema ya msimu wa Kilimo 2025/26 kwa kuandaa mbegu ili ziwafikie wakulima kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake, Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA), Boaz Ogolla amesema kuwa hadi mwishoni mwa wiki jana (August 17, 2025) wamenunua zaidi ya kilo Mil. 138 tofauti na mwaka jana, muda kama huo.
Ogolla amepongeza Mpango wa BBT kwa usimamizi mzuri wa zao hilo ambalo limeongeza ubora tofauti na miaka ya nyuma kwani taarifa za maabara ya Ubora wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba zinaonyesha ubora wa Pamba umeongezeka.
"Ubora wa Pamba wa mwaka huu umeongozeka, ukilinganisha na Ubora wa mwaka jana, taarifa ya Maabara kutoka Bodi ya Pamba imebadilika...BBT wameisaidia sana kusimamia na kudhibiti uchafuzi wa Pamba,.pia tumepata takwimu halisi za wakulima na mashamba yao" Amesema.
Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliances Ginnery, anaiomba serikali kupeleka Maafisa Ugani wa BBT kwenye kata ambazo hazikuwa na wataalamu hao ili waweze kuwasimamia wakulima katika msimu ujao.
Kuhusu viongozi wa Amcos kuchezea mizani, Ogolla aliiomba serikali kuwachukulia hatua kali ambao wamebainika kuchezea mizani ya pamba kwa lengo la kuwainia wakulima wa Pamba jambo ambalo ni tofauti na malengo ya Amcos kusimamia maslahi ya wakulima.
Kwa upande wao wakulima wa Pamba wameipongeza serikali kusimamia sekta ya Pamba kupitia Maafisa Ugani wa BBT ambao wameonyesha tija na mabadiliko ya uzalishaji.
Masunga Liki, mkazi wa Kijiji cha Nyanguge amesema kuwa Mpango huo umewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kutoka kilo 200 mpaka 300 walizokuwa wanazalisha kwa ekari moja na kufikia kilo 600 mpaka 800 kwa ekari.
Ameongeza kuwa wakulima hao wameona mabadiliko katika sekta ya Pamba na kushauri Elimu ya ugani, matumizi sahihi ya mbolea na Pembejeo yazingatiwe ili wakulima waongeze tija.
Naye Kundi Mashini, mkulima wa Pamba Kijiji cha Mhunze wilayani Itilima, ameiomba serikali kuwafikishia Matrekta ya serikali kwa wakati ili waweze kulima mapema wakiendana na kalenda ya Kilimo cha pamba.
Mwisho.
0 Comments