Marekani inazihimiza Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo kufikia makubaliano ya amani ambayo yataambatana na mkataba wa uwekezaji wa mabilioni ya dola katika madini, kwa mujibu wa mshauri mkuu wa Rais Donald Trump barani Afrika.
Shirika la habari la Reuters lilimnukuu Massad Boulos akisema siku ya Alhamisi: "Tutatia saini makubaliano ya amani...makubaliano ya madini na DRC yatatiwa saini siku hiyo, na yale yanayofanana na hayo, lakini yenye kiwango tofauti, yatatiwa saini na Rwanda siku hiyo hiyo."
Marekani na Qatar kwa muda mrefu zimekuwa zikifanya jitihada kubwa za kuleta amani kati ya nchi hizo mbili, kufuatia vita vya muda mrefu mashariki mwa Congo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini ambalo sasa lina miji mikubwa ya Goma na Bukavu inayodhibitiwa na waasi wa M23.
Katika mzozo huu, vikosi vya Rwanda vinashutumiwa kusaidia M23, wakati vikosi vya DRC vinashutumiwa kuwasaidia waasi wa FDLR wanaopigana na serikali ya Kigali. DRC na Rwanda zote zinakanusha hili.
Ijumaa hii, viongozi wa DRC na Rwanda wanatarajiwa kuwasilisha Washington tofauti maandishi ya awali ya makubaliano ya amani, ambayo yanatarajiwa kutiwa saini ndani ya miezi miwili, kulingana na Reuters.
Matunda ya mazungumzo haya ya amani yanaonekana kwani mapigano yamepungua kwa kiasi kikubwa katika wiki za hivi karibuni kati ya M23 na vikosi vya serikali na Wazalendo katika maeneo mbalimbali ya majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.
Boulos anasema kuwa kabla ya hafla ya kutia saini katika Ikulu ya White House, Washington inatarajia nchi hizo mbili kushughulikia maswala ya kila mmoja. Kwa mfano, kwamba Rwanda inapaswa kuondoa askari wake kutoka DRC na kuacha kuunga mkono M23. Na kwa upande wake DRC inapaswa kuondoa wasiwasi wa Rwanda kuhusu FDLR.
Kabla ya mkataba huo kutiwa saini, Boulos anasema kuwa Rwanda na DR Congo kwanza zitatia saini makubaliano ya kiuchumi na Washington ambayo yanajumuisha makampuni ya Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kuwekeza mabilioni ya dola katika uchimbaji madini katika migodi ya DR Congo, na miradi ya miundombinu kusaidia uchimbaji madini katika nchi zote mbili, ikiwa ni pamoja na usindikaji wa madini nchini Rwanda.
Boulos anasema kuwa makampuni ya Marekani na Magharibi yameiambia Washington kwamba yatawekeza mabilioni ya dola katika eneo hilo mara tu mikataba hii ya madini itakapotiwa saini.
0 Comments