Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewaagiza wachimbaji wa madini ya viwandani kuhakikisha wanayafukia mashimo yote yanayotokana na shughuli za uchimbaji ili kudhibiti uharibifu wa mazingira, hasa mmomonyoko wa ardhi unaotishia usalama wa wananchi katika maeneo husika.
Kauli hiyo imetolewa jana katika mkutano wa wadau wa madini ya viwandani (hasa Jasi, Pozolana, na Bauxite) kwa Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika wilayani Same. Mhe. Kasilda alisisitiza kuwa wachimbaji wote walioacha mashimo wazi wanapaswa kuyafukia mara moja ili maeneo hayo yaweze kutumika kwa shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Kuna maeneo mengi ambapo baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakiacha mashimo wazi baada ya kuchimba madini. Naagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro awatafute na kuhakikisha mashimo hayo yanafukiwa haraka, kwa kuwa yanahatarisha usalama wa wananchi na kuchochea uharibifu wa mazingira,” alisisitizaMhe. Kasilda.
Aidha, alieleza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kufuata sheria na taratibu zote za uchimbaji mara baada ya kupewa leseni, ikiwemo kujitambulisha kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri, Kata na Kijiji husika ili kuhakikisha shughuli zao hazihusiani na maeneo yenye migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, alisema mkutano huo umeitishwa kwa lengo la kuleta maazimio ya pamoja ya kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji. Alibainisha kuwa mkoa una zaidi ya wachimbaji 900 wenye leseni, zaidi ya watu 100 wana leseni za utafiti, na watu 40 wana leseni za biashara ya madini.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Bw. Emmanuel Bwambo, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji ni bei ndogo ya madini sokoni, jambo linalosababisha washindwe kugharamia shughuli za kufukia mashimo baada ya uchimbaji.
Katika mkutano huo, wadau walikubaliana kuwa na bei elekezi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wanunuzi wa madini ili kusaidia kufidia gharama za uzalishaji na kufukia mashimo. Pia walisisitiza umuhimu wa mashauriano kati ya wadau wa sekta ya madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Halmashauri katika kuhakikisha tozo na ushuru vinakuwa rafiki kwa wawekezaji.
Mhe. Kasilda aliagiza kuundwa kwa timu za ufuatiliaji zitakazojumuisha viongozi wa mitaa, maafisa mazingira, na wataalamu wa madini ili kuhakikisha masharti ya uchimbaji yanazingatiwa ipasavyo. Timu hizi pia zitatoa elimu kwa jamii kuhusu athari za mashimo ya wazi na umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Wadau walipendekeza kuanzishwa kwa programu za mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu uchimbaji endelevu, mbinu salama za kufukia mashimo, na usimamizi wa mazingira. Elimu hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa shughuli zao bila kuathiri mazingira au usalama wa jamii.
Ili kuhakikisha hatua za muda mrefu, mkutano huo pia uliibua wazo la kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuhifadhi mazingira utakaoshirikisha serikali, mashirika binafsi, na wachimbaji. Mfuko huo utasaidia kufadhili shughuli za urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa na kusimamia uendelevu wa sekta ya madini kwa maslahi ya wote.
0 Comments