NA BERDINA MAJINGE MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Wanafunzi wa fani ya Ununuzi na Ugavi katika Chuo Kikuu cha Iringa wametakiwa kuipenda taaluma yao kwa dhati, kwani kufanya kazi unayoipenda huongeza uwezekano wa kuitekeleza kwa weledi, uadilifu na uzingatiaji wa maadili.
Wito huo umetolewa na Afisa Masoko wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB), Dickson Mollel, wakati wa semina ya elimu kwa wanafunzi hao kuhusu majukumu ya bodi hiyo na umuhimu wa kufuata maadili ya taaluma hiyo.
Mollel alieleza kuwa kazi ya ununuzi inahusisha matumizi makubwa ya fedha za umma, hivyo ni muhimu kwa wataalamu wa fani hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka tamaa.
“Tunaendelea kutoa rai kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi kuzingatia maadili, waache tamaa ya utajiri wa haraka.
Kila mtu atafanikiwa kwa wakati wake endapo atafanya kazi kwa bidii na kwa kufuata taratibu,” alisema.
Alisisitiza kuwa kufanya kazi kwa moyo huongeza uwazi, usawa na kuepuka upendeleo, hasa ikizingatiwa kuwa serikali sasa inatumia mifumo ya kidijitali kusimamia mchakato wa manunuzi ya umma.
Aidha, Mollel aliwahimiza wanafunzi kujisajili rasmi na PSPTB ili watambulike kitaaluma mapema, jambo ambalo litawasaidia kujenga mtandao wa kitaaluma wakiwa bado vyuoni.
“Faida ya kujisajili ni kutambulika mapema na bodi. Pia inawarahisishia kujenga jina miongoni mwa wataalamu wa sekta yenu mnapohitimu,” aliongeza.
Naye Afisa Ununuzi kutoka PSPTB, Gabriel Mwakipesile, alisisitiza kuwa maadili ni nguzo muhimu katika kazi ya ununuzi kutokana na changamoto na vishawishi vinavyoukumba uwanja huo.
“Huwezi kufanya kazi za ununuzi na ugavi bila kutambulika na bodi. Msajiliwe ili bodi iweze kufuatilia mienendo yenu ya kitaaluma na kimaadili,” alisema.
Mbali na kusimamia maadili, Mollel alibainisha kuwa PSPTB ipo pia kwa ajili ya kuwatetea wataalamu wake pale inapohitajika, kwa kuwa inawafahamu rasmi na kuwatambua kisheria.
Baadhi ya wanafunzi walionesha ari ya kufuata ushauri huo na kujitambulisha rasmi na bodi.
Gladness Kawanga, mwanafunzi wa mwaka wa pili, alisema
“Niko tayari kujisajili na kufanya kazi kwa uadilifu bila upendeleo, kwa sababu fani hii naipenda kutoka moyoni.”
0 Comments