Header Ads Widget

BAADA YA TULIA, NSOMBA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA MBEYA MJINI



Siku moja tu baada ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, kutangaza kuachana na Jimbo la Mbeya Mjini na kuelekeza nguvu zake katika Jimbo la Uyole, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba, ametangaza rasmi nia ya kuwania ubunge wa jimbo hilo.


Akizungumza leo jijini Mbeya mbele ya waandishi wa habari, Nsomba amesema hatua hiyo imechochewa na wito kutoka kwa wananchi pamoja na uzoefu wake wa kiuongozi ndani ya chama.



“Ninafahamu changamoto za wananchi wa Mbeya Mjini, na nina dhamira ya kuzitatua kwa ushirikiano, uwazi na uwajibikaji,” alisema Nsomba huku akiahidi kusukuma mbele maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uchumi – hususan kwa vijana na wanawake.


Amesisitiza kuwa ushirikiano wake na Dk. Tulia utaendelea hata baada ya yeye kuelekeza nguvu Jimbo la Uyole, akiongeza kuwa ushindani ndani ya chama unapaswa kuwa huru na wa haki. “Natoa rai kwa wana CCM wenzangu wasiogope kutangaza nia endapo wamejipima. Chama chetu kitahakikisha haki inatendeka kwa wagombea wote,” alisisitiza.


Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa harakati za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika Jiji la Mbeya, huku nafasi ya Mbunge wa Mbeya Mjini ikifunguka kwa mara ya kwanza baada ya Dk. Tulia kuliongoza kwa miaka mitano.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI