Zaidi ya watu 400 wameuawa katika mashambulizi ya hivi majuzi ya Jeshi la Rapid Support Forces (RSF) katika jimbo la Darfur nchini Sudan, unasema Umoja wa Mataifa ukinukuu "vyanzo vya kuaminika".
Wiki iliyopita, RSF ilizindua mashambulizi makali ya ardhini na angani kwenye kambi za wakimbizi zinazozunguka mji wa El-Fasher katika jaribio la kuuteka mji mkuu wa mwisho wa jimbo la Darfur unaoshikiliwa na mpinzani wao, jeshi la Sudan.
Pande hizo mbili zinazozozana zimekuwa zimekuwa katika mapigano ya umwagaji damu tangu Aprili 2023. Hili limesababisha mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani na kuwalazimu mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao.
Umoja wa Mataifa ulisema kuwa umethibitisha mauaji 148 kati ya Alhamisi na Jumamosi, lakini ikaonya kuwa idadi hiyo ni kubwa zaidi.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani aliiambia BBC kuwa mchakato wao wa uhakiki bado unaendelea na idadi yao haijumuishi vurugu za Jumapili.
"Vyanzo vya kuaminika vimeripoti kuwa zaidi ya 400 wameuawa," alisema Bi Shamdasani.
Takriban wafanyakazi tisa wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu walikuwa miongoni mwa waliouawa, Umoja wa Mataifa ulisema.
Kambi za wakimbizi zinazozunguka El-Fasher - Zamzam na Abu Shouk - zinatoa makazi ya muda kwa zaidi ya watu 700,000, wengi wao wanakabiliwa na hali kama ya njaa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, RSF ilisema haihusiki na mashambulizi dhidi ya raia na kwamba matukio ya mauaji huko Zamzam yaliandaliwa kuharibia sifa vikosi vyake.
El-Fasher ni mji mkuu wa mwisho huko Darfur chini ya udhibiti wa jeshi na umekuwa ukizingirwa na RSF kwa mwaka mmoja. Vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vitaingia mwaka wake wa tatu Jumanne.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk alitoa wito kwa pande zote zinazohusika "kuingia katika makubaliano ya azimio jipya la kuchukua hatua katika kutatua mzozo".
0 Comments