Header Ads Widget

WIMBI LA WAFANYABIASHARA WA CHINA BARANI AFRIKA NI FURSA AU TISHIO KWA WAFANYABIASHARA WA NDANI?

 


Uwekezaji wa China barani Afrika umekuwa kwa kasi hasa maeneo ya miji mikubwa kama vile Dar es Salaam ambao umekuwa kitovu cha biashara.

Uwepo wa China katika masoko ya Afrika umekuwa miongoni mwa mielekeo muhimu zaidi ya kiuchumi katika karne ya 21.

Sio kuhusu miradi mikubwa ya miundombinu tu, ushawishi wa China unajidhihirisha pia kwa kina katika masoko ya ndani, mahusiano ya kibiashara, na shughuli za kila siku za biashara katika bara zima la Afrika.

Hii ni kutokana na miradi mbalimbali ya kimiundombinu kama vile Kituo cha Usafirishaji Kibiashara cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam Tanzania na kuongezeka kwa maduka na wauzaji wa rejareja ama jumla yanayomilikiwa ama kuendeshwa na Wachina jijini.

Ingawa makampuni ya biashara ya China yanaleta manufaa yasiyoweza kupingwa, kama vile bidhaa za bei nafuu kwa watumiaji, uundaji wa nafasi za kazi, na maendeleo makubwa ya miundombinu, pia yanaleta wasiwasi mkubwa kati ya wafanyabiashara wa ndani.

Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wa Kitanzania kwa mfano wanahisi kubanwa zaidi na ushindani, na kushindwa kuendana na bei ya chini na faida za mnyororo wa ugavi zinazofurahiwa na wenzao wa China.

Hali ya soko la China barani Afrika kwa ujumla

China ni mshirika mkubwa wa kibiashara barani Afrika. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, mahusiano ya kiuchumi kati ya pande hizi yameimarika kwa kasi kubwa kupitia mpango wa Forum on China, Africa Cooperation (FOCAC) ulioanzishwa mwaka 2000.

Kati ya mwaka 2000 hadi 2023, biashara kati ya China na Afrika imeongezeka kutoka chini ya USD 10 bilioni hadi zaidi ya USD 282 bilioni mwaka 2023 (UNCTAD, 2024).

China ni mnunuzi mkubwa wa malighafi kama mafuta kutoka Angola, madini kutoka DRC, na pamba kutoka Tanzania. Wakati huohuo, China huzisambazia nchi nyingi za Afrika bidhaa zilizotengenezwa kwa gharama nafuu kama nguo, vifaa vya kielektroniki, na mashine.

Kupitia ushirikiano huo wa kibiashara; Mauzo ya Afrika kuongezeka hasa ya bidhaa ghafi; manufaa kupitia Miundombinu: China imefadhili au kujenga zaidi ya 35% ya miradi ya miundombinu barani Afrika, ikiwemo barabara, reli (mfano SGR Kenya), na bandari.

Mbali na hiyo ni kutengeneza Ajira: Miradi hii pia imechangia ajira, ingawa mara nyingi kazi za juu hushikiliwa na Wachina wenyewe.

''Changamoto kubwa ninayoiona ni Afrika bado inasafirisha bidhaa ghafi huku ikinunua bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka China, hali hii huimarisha utegemezi. Pili ni Mzigo wa madeni kutokana na mikopo ya masharti nafuu kutoka China.'' Anasema Beatrice Kimaro, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi Tanzania.

Neema na tishio la wafanyabiashara wa Kichina Afrika


''Neema kwa nchi za Kiafrika inaonekana katika nyanja mbalimbali. Wafanyabiashara wa Kichina huleta teknolojia ya gharama nafuu (mfano mashine za kilimo, mashine ndogo za viwanda), Miradi ya Wachina huajiri wafanyakazi wa ndani (mfano katika ujenzi wa barabara na majengo)''.

''Pia ushindani wa bei kwa kuwa bidhaa zao ni nafuu hivyo zinawasaidia wateja wa kipato cha chini kupata mahitaji yao kwa bei rafiki.'' Anasema Beatrice.

Dotto Sedekia ni mfanyabiashara 'machinga' anauza bidhaa mchanganyiko, jijini Dar es Salaam anasema kwao kwa kiasi kikubwa uwepo wa Wachina umewanufaisha

''Wachina wamefanya wafanyabiashara wenye misingi midogo kunyanyuka, kutokana na unafuu wa gharama za bidhaa zao, mfanyabiashara anaweza kuchukua mzigo kwa bei nafuu na hata kumkopesha na wanalipa, kwa kweli wameleta ushindani wa kibiashara.''

Tishio kwa Wafanyabiashara wa Ndani;

Uhodhi wa Soko: Wachina wengi huingia hadi katika ngazi ya rejareja na kuuza sokoni bidhaa walizozileta wao wenyewe, wakipunguza faida ya wafanyabiashara wa ndani.

Kukosa Ushindani wa Bei: Bidhaa zao huwa ni bei ya chini kutokana na uzalishaji mkubwa na ruzuku kutoka serikalini, hivyo wafanyabiashara wa ndani hushindwa kuhimili ushindani.

Wanaendesha biashara kwa mikataba isiyo rasmi au bila leseni, jambo linalovuruga ushindani wa haki.

Malalamiko ya wafanyabiashara wa ndani


Malalamiko Mahususi katika masoko mbalimbali yamekuwepo kwa wingi (Mfano Tanzania):

Wachina kuingia biashara za rejareja, ambazo kisheria zinapaswa kuwa kwa wazawa pekee.Wameingia hadi kwenye maduka makubwa na madogo ya bidhaa mbalimbali.

Wanaanzisha biashara bila kuzingatia utaratibu wa leseni au usajili.

Wanaajiri watu wachache sana wa ndani au kuendesha biashara kama familia bila kutoa ajira. Haya ni malalamiko ya mida mrefu, yako Tanzania, Kenya, Ghana, Gambia na nchi nyingi za Afrika.

Kwa sababu hiyo, Serikali ya Tanzania iliunda kamati ya watu 15 kuchunguza mazingira ya wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya biashara za wazawa katika soko la kimataifa la biashara la Kariakoo wakiwemo Wachina.

Soko la Kariakoo limekuwa na ongezeko la maduka ya Wachina wakifanya biashara ya nguo, vifaa vya nyumbani n.k.

''Sisi wenyewe wazawa tunapouziana tofauti yake inakuwa kubwa sana, lazima utakimbilia kwa Mchina, sasa wafanyabiashara wakubwa wa Kitanzania wanaona hawapati faida kwasababu wamezoea bei kandamizi'' Anaeleza mfanyabiashara mdogo, Sedekia

Soko la Karume na Mbagala, kuna ushindani mkali kutoka kwa Wachina wanaouza bidhaa moja kwa moja kwa wateja, jambo linalozua malalamiko.

Nini kifanyike kulinda soko la ndani?

"Kwa jinsi ilivyo malalamiko yataendelea, kwa sababu bidhaa wanazoziuza wachinanyingi ni kutoka kwao, wanazitengeneza wao, najiuliza unalindaje bidhaa usizokuwa nazo? Ushindani muhimu ni kutengeneza bidhaa kama zao, kwa viwango, utalinda soko na wazalishaji wako wa ndani", anasema Yusuph Mazimu, Mwandishi wa BBC wa habari za Uchumi na biashara.

Nchi za Kiafrika pia zinapaswa kupitisha sera zinazolenga kuleta ufadhili wa siku zijazo wa ukuaji wa uchumi. Kudorora kwa uchumi wa China kunaweza kuibua kasi ya ukuaji wa Afrika kwa kubana uwezo wa kifedha wa miradi mikubwa kutokana na uwezekano wa kuimarika kwa mikopo ya biashara na uwekezaji kutoka kwa benki za China zinazoshiriki kikamilifu barani Afrika.

Katika suala hili, biashara ya ndani ya Afrika na ufadhili wa uwekezaji kutoka kwa taasisi za kifedha za kikanda ikijumuisha Benki ya Maendeleo ya Afrika inaweza kutoa fursa ya kutengemaa fedha za muda mrefu. Wataalam wa biashara na uchumi wanapendekeza mambo kadhaa.

1. Marekebisho ya Sera na Utekelezaji:

Serikali zinapaswa kuhakikisha sheria za uwekezaji zinazingatia biashara za ngazi ya chini kuwa ni kwa wazawa pekee mfano wa Rwanda na Botswana.

Pia kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vibali vya kazi na biashara.

2. Kuwekeza kwa Wazawa;

Serikali ziweke mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa ndani kupitia mikopo nafuu, elimu ya ujasiriamali, na upatikanaji wa masoko.

3. Ubunifu na Ushindani;

Wazawa wahamasishwe kubuni bidhaa zenye ubora, kuungana katika vikundi kama (SACCOS, AMCOS) vilivyo Tanzania ili kununua kwa pamoja na kupata nguvu ya ushindani.

4. Ulinzi wa Kibiashara;

Ziwepo tozo maalumu kwa bidhaa za bei ya chini kutoka nje na vibali maalumu kwa biashara zinazopaswa kufanywa na wawekezaji wa kigeni, kuhakikisha wanawekeza mitaji mikubwa na kutoa ajira kwa wazawa.

Uwepo wa China barani Afrika ni na fursa na changamoto. Ushirikiano wa kiuchumi na China unaweza kuleta maendeleo iwapo utasimamiwa kwa uwazi, usawa, na kwa kuzingatia maslahi ya ndani.

Kupitia sera madhubuti, uwekezaji katika biashara za wazawa, na utekelezaji wa sheria, Afrika inaweza kufaidika na ushirikiano huu bila kuumiza biashara za ndani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI