Header Ads Widget

UMOJA WA CHODA HURU WAIPIGA TAFU VITENDEA KAZI SHULE YA MSINGI CHODA

 

Na Thobias Mwanakatwe,Habari na Matukio App,IKUNGI 

UMOJA wa Wanafunzi Waliosoma katika Shule ya Msingi Choda (CHODA HURU) iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida umeipiga tafu shule hiyo kwa kuipatia kompyuta, mashine ya kudurufu karatasi (photocopy mashine) na limu ya karatasi.

Mweka Hazina wa umoja huo unaoundwa na wanafunzi 18 waliohitimu katika shule hiyo kwa miaka tofauti, Fadhili Singisi, akikabidhi vifaa hivyo hivi karibuni alisema wameamua kutoa vifaa hivyo ili kuwasaidia walimu na wanafunzi kuondokana na adha waliyokuwa wanaipata katika utendaji wao wa kazi.

Singisi amesema umoja huo unatambua umuhimu wa shule hiyo na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya elimu nchini lakini na wao kama wadau wameona umuhimu wa kuisaidia shule hiyo.

"Shule ya Msingi Choda tumesoma hapa kwa hiyo tumeona turudishe fadhili kwa kusoma hapa manaa ndipo ramani ya maisha yetu ilianzia hapa  na tunashukru sana kwa jinsi ambavyo serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika shule hii," amesema Singisi.


Singisi ameongeza kuwa darasa moja ambalo lina changamoto, umoja huo utaendelea kukusanya nguvu ya kifedha ili kuangalia namna ya kulikarabati liweze kuwa katika mazingira yatakayowawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.


"Serikali haiwezi kufanya kila kitu kwa hiyo sisi kama wadau binafsi tunastahili kusaidiana na serikali yetu katika mikakati ya kuboresha elimu nchini kwa hiyo niwaombe wadau wengine hususani waliosoma katika Shule ya Msingi Choda kuikumbuka shule hii kwa kuipatia misaada mbalimbali," amesema Singisi.



Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Choda,Gerald Luwoga akipokea vifaa hivyo aliwa ba Afisa Elimu Kata, alishukru kwa msaada wa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kurahisisha utungaji mitihani kwa njia ya kisasa.

Amesema wamekuwa wakipata changamoto ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 40 kwenda Manyoni au Ikungi mjini kwa ajili ya kwenda kuchapa au kutoa nyaraka mbalimbali za shule  na hivyo kuingia gharama kubwa.


"Kutokana na umbali wa kutoka shuleni kwetu kwenda mjini tulikuwa tunalazimika mitihani tukishaitunga tunawaandikia ubaoni wanafunzi kwasababu kuchapa kwenye karatasi ni changamoto lakini sasa uwepo wa vifaa hivi utawarahisishia utendaji kazi," amesema.


Kwa upande wao wanafunzi wa shule hiyo walisema wanalazimika kutembea urefu wa zaidi ya kilometa 10 kufuata shule ambayo ipo mbali na vitongoni vyao na kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga shule nyingine ambayo itakuwa karibu na vitongoji vyao ambavyo vipo vitano.

 Afisa Elimu Mkoa wa Singida,Dk. Elipidius Baganda, alipoulizwa kuhusu changamoto baadhi ya vijiji wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule alisema serikali inaendelea na mkakati wa kujenga ambazo zitakuwa karibu na mazingira ya wananchi.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI