Header Ads Widget

KASI YA UPANUZI WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE MUSOMA WAMRIDHISHA RC MTAMBI

 

Na Shomari Binda ,Matukio Daima Media,Musoma 

MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameipongeza TANROADS mkoa wa Mara kwa usimamizi mzuri na kasi ya upanuzi wa uwanja wa ndege Musoma.


Licha ya pongezi hizo ametoa maelekezo ya kuhakikisha uwanja huo unakamilika septemba mwaka huu na kuanza kutoa huduma.


Pongezi na maelekezo hayo ameyatoa jana aprili 11,2025 alipotembelea uwanja huo na kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa uwanja huo.


Amesema taasisi zote zinazohusika na mradi huo kuhakikisha unakamilika kabla ya septemba 2025 ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.





Mtambi tayari serikali imetoa fedha za ukamilishaji wa uwanja huo na kwa kasi aliyoiona katika uwanja huo haoni sababu kutokukamilika mapema. 


“Taarifa yenu na hali halisi ya utekelezaji wa mradi huu inaonyesha kuwa unaweza kukamilika kabla ya septemba angalieni mtakachoweza kufanya ili mradi huu ukamilike mapema kutokana na umuhimu wake kwa mkoa wa Mara.


"Uwanja huu utakapokamilika utasaidia sana katika kuwasafirisha wananchi, watalii, madini, samaki na mizigo mingine kutoka mkoa wa Mara kwa urahisi na haraka na utasaidia katika kukuza uchumi wa mkoa wa Mara",amesema.


Mkuu huyo wa mkoa amemtaka mkandarasi wa mradi huo kukamilisha shughuli zilizobakia ili uwanja uweze kutumika kwa muda uliokusudìwa.


Aidha amemtaka meneja wa uwanja wa ndege Musoma kufuatilia mchakato wa ujenzi wa majengo mapya ya abiria kwa ukaribu huku akiendelea kufanya maandalizi ya kuanza kupokea ndege za abiria katika majengo ya zamani ya yaliyopo katika uwanja huo.

Maelekezo mengine yametolewa kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka kufuatilia utekelezaji wa mradi huo kwa karibu na kuongeza kuwa mradi huo ukikamilika utaichangamsha sana Manispaa ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla kibiashara na utalii. 

 Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe amesema awali mradi huo ulisimama kutokana na mkandarasi kudai malipo yake baada ya kukamilisha sehemu ya kazi lakini kwa sasa ameshalipwa asilimia 80 ya fedha zote na anaendelea na ukamilishaji wa mradi. 

“Utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 58 ya utekelezaji wa jumla wa mradi huu na tunatarajia kuukamilisha mwezi septemba mwaka huu”, amesema mhandisi Maribe. 

Amesema wananchi wote waliotakiwa kulipwa fidia ili kupisha mradi wameshalipwa na wanaendelea na maandalizi ya kuhama katika eneo hilo ili upanuzi wa uwanja huo uweze kuendelea.  

Kwa upande wake meneja wa uwanja wa ndege Musoma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Frank Msofe amesema taratibu za kukarabati na kuweka sawa majengo yaliyopo kwa ajili ya kutumika kupokea abiria zinaendelea wakati wakisubiria ujenzi wa majengo ya kisasa ya abiria katika uwanja huo. 

Amesema tayari serikali imeanza mchakato wa kuwalipa wananchi 58 fidia ya zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kupisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya kupokelea abiria katika uwanja huo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI