Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
UMOJA wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) Kanda ya Kati, umeitaka serikali kulitafutia ufumbuzi tatizo la shule mpya zinazofunguliwa kucheleweshewa kupata fedha za ruzuku ya uendeshaji kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi bila Ada hali inayoathiri taaluma katika shule hizo.
Mwenyekiti wa TAHOSA Kanda ya Kati, Jeremia Mungwe, amesema hayo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa umoja huo unaofanyika katika Manispaa ya Singida na kuwashirikisha wakuu wa shule zaidi 400 kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.
"Hali ya taaluma katika mikoa yetu inaendelea kuimarika sana lakini pamoja na mafanikio haya bado kuna changamoto ya shule mpya kuchelewa kupata fedha za ruzuku ya uendeshaji kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi bila ada," alisema," amesema Mungwe.
Mungwe amesema changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya elimu ni ushirikiano hafifu wa baadhi ya wazazi katika utekelezaji wa mkakati wa kuinua ufaulu ikiwamo utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi na kuendelea kuwepo kwa tatizo la utoro na mdondoko wa wanafunzi mashuleni.
"Tunampongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha elimu yetu nchini, wakuu hawa wa shule ni mashahidi fedha nyingi zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa,vyoo,shule mpya na ukarabati wa shule," amesema Mungwe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego, akifungua mkutano huo aliwataka walimu kuendelea na malezi kwa wanafunzi na kwamba katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia linahitaji ubunifu katika kusimamia maadili ya watoto.
"Suala la maadili limekuwa changamoto sana kwa watoto sasa hivi watoto wetu wanalelewa na facebook, Instagram na mitandao mingine msiwachekee watoto wetu wanasema samaki mkunje angali mbichi akishakua hakunjiki,"alisema.
Dendego amesema serikali itaendelea kushughulikia changamoto za walimu ikiwamo madai,kupandishwa madaraja,kuajiri walimu,kujenga nyumba za walimu na stahiki mbalimbali ili walimu wafanye kazi kwa uzalendo na kuleta matokeo tarajiwa.
Amesema walimu kwa kutumia jukwaa la TAHOSA kujadili kwa kina na kupeana uzoefu wa namna ya kusimamia na kufanya ufuatiliaji wa kutekelezaji wa mikakati ya kuinua ufaulu iliyoandaliwa na mikoa pamoja na halmashauri.
"Wakuu wa shule mnalo jukumu kubwa la kusimamia hatua ya mwisho ya utekelezaji wa mikakati na bila usimamizi makini hatuwezi kufikia malengo," amesema Dendego.
Ameongeza kuwa wakuu wa shule waendelee kusimamia miradi ya ujenzi kizalendo na kikamilifu ili thamani ya fedha ionekane na kupata miundombinu bora kama ilivyokusudiwa.
Dendego amewakumbusha walimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu hasa wazazi kushiriki katika utekelezaji wa mikakati ya ufaulu ikiwemo utoaji chakula cha mchana kwa wanafunzi ili wapete utulivu na kuongeza uelewa wanapofundishwa wakiwa wameshiba.
"Kila mmoja wenu awe na kiu ya kutaka kupata matokeo mazuri ya shule yake,ufaulu wa shule zote ndio utaifanya mikoa yetu ipande kitaaluma, haya yote yatafanikiwa ikiwa mtashirikiana katika kila hatua mnapowaandaa watoto katika ufundishaji na malezi kwa ujumla," alisema.
Mkuu wa Mkoa amesema serikali kupitia kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya elimu nchini.
"Rais Dk.Samia katika kipindi chake amefanya mambo makubwa sana katika sekta ya elimu kwa kujenga vyumba bora vya madarasa,matundu ya vyoo,nyumba za walimu na ukarabati wa shule kongwe kote nchini,"amesema Dendego.
MWISHO
0 Comments