Simba imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF baada ya kuiondoa Al Masry ya Misri kwa mikwaju ya penati 4-1 kwenye mchezo pili wa robo fainali uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo wa kwanza kule Misri, Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0, ambapo Jijini Dar es Salaam Simba ilirejesha mabao hao, kupitia kwa Elie Mpanzu na Steven Mukwala.
Shomari Kapombe alifunga penati ya ushindi huku Mlinda mlango Moussa Camara akiibuka nyota wa mchezo wa kuokoa mikwaju miwili ya penati.
Kabla ya Mchezo wa leo, simba ilikuwa inaitwa mwakarobo na watani zao Yanga kwa kushindwa kuvuka robo fainali mara kwa mara. Kati ya robo fainali 7 kabla ya hii ya sasa, ilikuwa imefanikiwa kuvuka mara mbili tu hatua hiyo.
"Simba ajiandae kutoka, abakie Mwakarobo, tuendele kubakia na lile jina, na pale Mwakarobo hawezi kutoka, ni Mwakarobo, nusu haiwezekani, Simba uwezo hana."
Hii ilikuwa kauli ya mzaha kutoka kwa mmoja wa mashabiki wa Yanga alipozungumza na chombo kimoja cha Habari Tanzania, akiwatania watani wao wa jadi Simba SC, kufuatia kipigo cha 2-0 kutoka kwa Al Masry kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, kule Misri.
Katika soka la Tanzania, majibizano ya mashabiki wa Yanga na Simba si jambo geni, lakini jina la "Mwakarobo" limejikita zaidi katika simulizi ya maumivu ya mara kwa mara ya Simba kutolewa kwenye hatua ya robo fainali. Mwakarobo ni jina la kawaida tu la asili ya watu wa Mkoa wa Mbeya, hasa Tukuyu.
Sasa, tarehe 9 Aprili 2025, Simba imeingia dimbani Benjamin Mkapa kurudiana na Al Masry, na kuichapa 2-0 na kufanya matokeo kuwa 2-2, kabla ya kwenda kwenye mikwaju ya penati na kushinda mikwaju 4-1.
Zimwi la Mwakarobo ndiyo basi tena Simba?
Kabla ya mchezo wa April 9, 2025, katika historia yake tangu kuanzishwa mwaka 1936, Simba SC imewahi kufika robo fainali ya mashindano ya Afrika mara nane, kwenye michuano mbalimbali ikiwemo Kombe la Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), Kombe la CAF, na Kombe la Shirikisho. Cha kushangaza, katika mara hizo zote nane, ilikuwa imevuka hatua ya robo fainali mara mbili tu.
Mara ya kwanza kilikuwa mwaka 1974, Simba ilipowatoa Hearts of Oak ya Ghana kwa jumla ya mabao 2-0 ugenini mjini Accra, Ghana kwa mabao ya Abdallah 'King' Kibadeni na Adam Sabu, kabla ya Kwenda sare tasa ya 0-0 jijini Dar es Salaam. Kikosi cha Simba kilikuwa na magwiji kama 'King' Kibadeni, Sabu, Mohamed Kajole, Athuman Mambosasa, na Abbas Dilunga. Hii ilikuwa ni enzi ambazo hata mfadhili mkubwa wa sasa wa klabu, Mohammed "Mo" Dewji, alikuwa hajazaliwa.
Hata hivyo, katika hatua ya nusu fainali, Simba walikumbana na Mehala El Kubra ya Misri na kupoteza nyumbani 1-0 na kisha kipigo kama hicho ugenini na kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Simba ilivuka tena robo fainali mwaka 1993, safari hii dhidi ya Al Harrach ya Algeria. Iliibuka na ushindi wa 3-0 nyumbani kwa mabao mawili kutoka kwa Edward Chumila "Edo" na moja kutoka kwa Ramadhani Abdul "Mashine", kabla ya kupoteza 2-0 ugenini. Hii ilikuwa enzi ambazo msemaji wa sasa wa klabu, Ahmed Ally, alikuwa bado mtoto wa darasa la kwanza au pili au hajaanza shule kabisa.
Baada ya hapo, Simba iliitoa Atletico Sport Aviacao ya Angola nusu fainali na kufika fainali, ambako walikumbana na Stella Abidjan ya Ivory Coast na kupoteza jumla ya mabao 2-0.
Hizi ndizo nusu fainali mbili pekee ambazo Simba imewahi kuzifikia kwa karne karibu tisa tangu kuanzishwa kwake. Mara nyingine zote, hatua ya robo fainali imekuwa kama ukuta wa chuma.
Katika Kombe la Klabu Bingwa Afrika (zamani), Simba ilishiriki mara 9 na kufika robo fainali mara mbili, mwaka 1974 walipovuka na 1994 walipoishia hapo.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo ni toleo jipya la mashindano hayo, Simba wameshiriki mara 9 pia, na kufika robo fainali mara nne, katika misimu ya 2018/2019, 2020/2021, 2022/2023, na 2023/2024, lakini bila kuvuka Kwenda nusu.
Katika Kombe la Shirikisho la CAF, Simba wameshiriki mara 7 hadi sasa, na hii ya 2024/2025 ni robo fainali yao ya pili katika michuano hiyo, baada ya ile ya 2021/2022.
Kwa kufuzu nusu fainali sasa, je ni mwisho wa jina la Mwakarobo?
Zimwi hili linawatisha Simba?
Beki Mcongo wa Simba, Henock Inonga Baka (kulia) akiwania mpira na mshambuliaji wa Wydad, Msenegali, Sambou Junior wakati wa mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Wydad AC na Simba SC kwenye Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca, Aprili 28, 2023. Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penati.Licha ya rekodi hiyo ya kukwama kufika robo fainali mara kwa mara, tangu mwaka 2018 hadi sasa, Simba SC imefanikiwa kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi kimataifa kutoka Afrika Mashariki kwa kufika robo fainali sita katika mashindano makubwa barani Afrika.
Kwa kiwango hicho, bila shaka Simba ni mabingwa wa kweli wa ukanda huu. Kwa rekodi ya kufika robo faibali, simba inastahili sifa, ni hatua kubwa imepiga katika miaka ya hivi karibuni. Watani zao Yanga wao wanajivunia kuingia fainali ya kombe la shirikilo, CAF, msimu wa 2022/2023.
Lakini mashabiki wa Simba hawatosheki na robo fainali tu. Walikuwa wanataka hatua kubwa zaidi. Na sasa jina la Mwakarobo linaweza kuwa historia kwao.
Simba itapindua meza kwa Mkapa?
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa na wachezaji na viongozi wa Simba. Klabu hiyo, kama ilivyokuwa kwa Yanga imekuwa ikipata uungwaji mkono na Serikali kwenye michuano ya Kimataifa.Simba itapindua meza kwa Mkapa? lilikuwa swali kubwa kwa mashabiki wa soka la Tanzania. Simba SC ilikabiliwa na kazi ngumu ya kugeuza matokeo baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Al Masry huko Misri. Ushindi wa April 09, 2025 unaipeleka simba nusu fainali ya tatu ya soka la Afrika tangu kuanzishwa kwake. Ilikuwa hali ni ngumu, lakini si ngeni kwa Simba.
Mwaka 1979, Simba ilifanya moja ya miujiza mikubwa kwenye historia ya soka la Afrika: ilifungwa 4-0 nyumbani na Mufulira Wanderers ya Zambia, lakini ikapindua meza kwa kishindo ugenini kwa kuishinda 5-0 na kufuzu hatua inayofuata, ingawa haikuwa ya nusu fainali.
Katika miaka ya karibuni zaidi, msimu wa 2018/2019 wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilifungwa 2-1 na Nkana FC ugenini, lakini ilishinda 3-1 kwenye dimba la Benjamin Mkapa na kufuzu hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-3. Ni katika uwanja huu huu walipoandikwa mashujaa.
Aidha, Simba ina rekodi nzuri ya kutopoteza nyumbani: katika mechi 10 za mwisho za Afrika zilizopigwa jijini Dar es Salaam kabla wa Al Masry, Simba imepoteza mechi moja tu dhidi ya Al Ahly ya Misri. Almanusura pia ipindue mezi iliposhinda mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kwenye robo fainali ya klabu Bingwa Afrika. Kama si ushindi mnono wa mabao 4-0 walioupata Waafrika Kusini hao, kwenye mechi ya kwanza katika uwanja wa FNB Jijini Johannesburg.
Ingawa haiko tena enzi za King Kibadeni, Edward Chumila, au hata mastaa wa miaka ya hivi karibuni kama Luis Miquissone, John Bocco na Clatous Chama, Simba inajivunia vipaji kama Charles Ahoua, Fabrice Ngoma, Elie Mpanzu, pamoja na wazoefu wa mashindano ya Afrika kama Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala'.
Sasa, mbele ya mashabiki wao, ndani ya jiji lao, kwenye ardhi yao, Smba imeweza kufuzu nusu fainali, Je italiondoa jina la Mwakarobo midomoni mwa watani wao kwa kuendelea mpaka fainali?
0 Comments