Na Fatma Ally Matukio Daima App
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameahidi kutoa shilling mill 100 kwa ajili ujenzi wa Zahanati ya Saranga kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Kibamba sambamba na kuskiliza kero za wananchi ikiwemo afya, maji, barabara pamoja na Tasaf.
Amesema kuwa, licha ya Rais Dkt Samia kutoa fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya Afya kwa kujenga hospital kubwa, kuongeza madaktari bingwa na kuongeza vifaa tiba lakini hajawaacha wananchi wa Kata ya Saranga.
Aidha, amemtaka fundi ujenzi aliyejenga kituo cha Afya cha mama na mtoto Mpigi Magoe kufanya marekebisho ya dosari alizozigundua mara moja kabla ya kumchukulia hatua za kumpeleka gerezani akajenge milango ya magereza.
"Ukiondoa taaluma yangu, pia ninauwelewa wa masuala ya ufundi, hivyo kwa kuangalia tu, yapo baadhi ya makosa ambayo tayari nimeelekeza uyafanyie kazi, nitarudi tena bila taarifa nikikuta hujarekebisha basi itabidi upelekwe gerezani maana kule kuna milango imeharibika"
Katika hatua nyengine ametoa maagizo kwa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (DAWASA) mkoani humo ambao umegharimu shill bill 36.8 kuanza mchakato wa kuzalisha umeme utakaotumika katika mashine za kusambazia maji ili kupunguza gharama.
Ameongeza kuwa, kwa sasa Dawasa inatumia bil. 2 kuilipa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) bil ya umeme, hivyo inaweza kuepuka gharama hiyo ikiwa itazalisha umeme wake na Tanesco itumike kusambaza tu.
"Kuona mradi huu umeanza kufanya kazi , kwetu ni mafanikio makubwa na tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu.
"Hivyo huu si muda wa kudanyanyana kama sehemu kuna tatizo, kiongozi husika anatakiwa kusema ukweli ili Serikali itoe fedha, nikigundua kuna kiongozi hajasema ukweli kama kuna sehemu kuna tatizo ili wananchi wasaidiwe na nikabaini nitaanza na yeye," amesema.
Aidha, RC Chalamila ameagiza miradi yote iendane na thamani ya fedha unayotolewa katika Jimbo la Kibamba wilaya ya Ubungo na kuagiza miradi hiyo kujengwa kwa viwango na kuzingatia thamani ya fedha, ambapo ameagiza miradi hiyo kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,, Lazaro Twange, amesema kwamba kukamilika kwa mradi wa maji Kibamba kutanufaisha kuondoa changamoto ya ukosefu ya maji katika Kata za jimbo hilo.
Pia Diwani wa Kata ya Kwembe, Nicolus Batiligaya amesema mwaka 2020, kata yake ilikuwa na ukosefu wa maji na sasa wananchi wake wanapata huduma hiyo kwa asilimia 90.
"Natoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ujenzi wa miundombinu ya maji ambayo imeboresha maisha ya wananchi wangu kupata maji safi na salama na kuwepo utofauti mkubwa na miaka mitano iliyopita, " amesema.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Juma Japhari Nyaigesha amewataka wananchi na wafanyabiashara kuto kukwepa kulipa kodi kwani ndio chanzo cha kupata fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo vituo vya afya huku Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Mpiji Magoe Hereswida Cosmas akieleza maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la mama na mtoto amesema ujenzi unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati.
Aidha Katika ziara hiyo wilayani Ubungo RC Chalamila pia ametembelea na kukagua mradi wa maji wa kibamba, pamoja na kukagua mradi wa shule ya sekondari goba kulangwa.
0 Comments