Na Matukio Daima
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye Sekta ya Afya kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo ujulikanao kama Samia Health Super-Specialization Program, ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/26 imetenga jumla ya Shilingi Bilioni tisa (9) kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi kwa wataalam wa afya.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Agosti 21, 2025 katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijiji Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mpango huo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Waziri Mhagama amesema Mpango huo unaosimamiwa na Wizara ya Afya utawezesha watumishi wa afya kupatiwa ufadhili wa masomo ya kibingwa kwa fani zenye uhitaji mkubwa ambapo utahusisha ufadhili wa ada, nauli, posho ya utafiti na posho ya kujikimu kwa wanaosoma ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na Wizara ya Afya. kwa mwaka wa fedha 2025/26.
"Mpango huu maalum unalenga kusomesha angalau wataalam 300 wa afya kila mwaka katika fani mbalimbali zenye kipaumbele kwa seti, hatua inayolenga kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi, kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi na kuvutia tiba utalii," amesema Waziri Mhagama.
Kuhusu dirisha la maombi Waziri Mhagama amefafanua kuwa limefunguliwa rasmi kuanzia Agosti 20, 2025 hadi Septemba 12, 2025 na maombi yanapaswa kuwasilishwa kwa njia ya kielektroniki pekee kupitia tovuti ya Wizara ya Afya: https://esponsorship.moh.go.tz na maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yatakayowasilishwa kwa njia ya mfumo huo pekee.
Pia amesema vigezo vya kupata ufadhili vimeelezwa kwa kina katika tangazo rasmi kwenye tovuti ya Wizara ya Afya, miongoni mwavyo ni mwombaji kuwa mtumishi wa Serikali, raia wa Tanzania, awe amepata udahili kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali, na awe anakwenda kusomea fani zenye kipaumbele kulingana na uhitaji wa kituo chake cha kazi.
Mwisho Waziri Mhagama ametoa wito kwa waombaji wote kufuatilia tangazo lililopo katika tovuti ya wizara kwa anwani ya www.moh.go.tz kuwa makini na kuhakikisha wanatimiza masharti yaliyowekwa kwa niaba ya Sekta ya Afya.
0 Comments