Header Ads Widget

RC CHONGOLO AZINDUA UTOLEWAJI HUDUMA ZAHANATI YA MTIMA

Na Moses Ng'wat, Ileje.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, leo Aprili 9, 2025 amezindua rasmi utolewaji huduma katika Zahanati ya Kijiji cha Mtima, Kata ya Mbebe, Wilayani  Ileje, ambapo amewapongeza wananchi kwa mshikamano wao uliowezesha ujenzi wa kituo hicho muhimu cha huduma za afya.


Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Chongolo amesema mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 120.4, ambapo wananchi wamechangia zaidi ya shilingi milioni 20, ikiwemo nguvu kazi na ujenzi wa boma la zahanati hiyo.


“Wananchi mmeonesha uzalendo wa hali ya juu. Serikali inatambua jitihada zenu na itaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia kwa ukaribu zaidi,” alisema Chongolo.


Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya ili kuboresha maisha ya wananchi.


Hata hivyo, aliwataka wananchi waepuke siasa za chuki na uchochezi zinazolenga kudhoofisha jitihada za maendeleo.


“Tanzania imejengwa katika misingi ya amani na mshikamano. Tuendelee kuwa waangalifu dhidi ya wanasiasa wanaotaka kuchafua taswira ya serikali na kuharibu umoja wetu,” alisisitiza Chongolo.


Akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Dkt. Arnold Musiba, amesema mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ufadhili wa serikali kuu na ushirikiano wa wananchi.


Dkt. Musiba amesema kati ya shilingi milioni 120.4 zilizotumika, serikali imetoa milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji na kiasi kingine cha milioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.


“Tayari tumepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 22.88 na huduma zimeanza kutolewa, ikiwemo kliniki ya mama na mtoto, OPD, huduma za uzazi, dawa, ushauri nasaha, na huduma tembezi na hadi sasa wateja 81 wamehudumiwa,” alisema Dkt. Musiba.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happness Seneda, alisisitiza umuhimu wa utunzaji sahihi wa nyaraka za miradi ili kusaidia viongozi na wakaguzi kuthibitisha thamani halisi ya miradi inayotekelezwa.


Uzinduzi huo umeonesha dhamira ya serikali katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, sambamba na kuwashirikisha katika maendeleo ya jamii zao.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI