Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague imeanza kusikiliza kesi ya Sudan dhidi ya UAE kwa tuhuma za kuunga mkono vikosi vya Rapid Support Forces ambayo imekuwa ikipigana nayo tangu katikati ya Aprili 2023.
Mahakama hiyo imepanga vikao viwili ambavyo vitazingatia ombi la Sudan la hatua za dharura kuchukuliwa dhidi ya UAE, ambayo inasema imekiuka Makubaliano ya Kimbari kuhusu watu wa Masalit, haswa huko Darfur Magharibi.
Katika ombi lake kwa ICJ, Sudan inadai RSF imekuwa na hatia ya "mauaji ya kimbari, ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia, uhamishaji wa lazima, na ukiukaji wa haki za binadamu."
Inadai: "Vitendo vyote kama hivyo vimetekelezwa na kuwezeshwa na msaada wa moja kwa moja kwa waasi wa RSF na nchi ya Falme za Kiarabu.
Sudan pia imewasilisha malalamiko dhidi ya taifa hilo la Ghuba katika Baraza la Usalama la UN.
Hata hivyo, UAE, imetupilia mbali madai hayo. Waziri wake wa Mambo ya nje, Anwar Gargash, katika ujumbe kwenye mtandao wa X, alisema "kipaumbele cha Sudan kinapaswa kuwa kusitisha mapigano katika vita hii ya upuuzi na ya uharibifu - na kushughulikia janga kubwa la kibinadamu ambalo limejitokeza."
Mnamo mwezi Januari, Marekani iliamua kwa kauli moja kwamba vikosi vya Rapid Support Force (RSF) - vilijihusisha katika vita vya kikatili dhidi ya vikosi vya jeshi la Sudan tangu 2023 - walikuwa na hatia ya mauaji ya kimbari na kuamuru vikwazo dhidi ya Kamanda Mohammed Hamdan Dagalo.
0 Comments