Header Ads Widget

MAREKANI YAWAFUNGULIA MASHTAKA RAIA WAKE WALIOTUHUMIWA KUFANYA JARIBIO LA MAPINDUZI DRC

Raia wa Marekani waliohukumiwa kwa kuhusika katika mapinduzi yaliyofeli nchini DRC

Wizara ya Sheria ya Marekani imewafungulia mashtaka raia wanne wa Marekani kwa kuhusika kwao katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya watatu kati yao kurejeshwa mikononi mwa mamlaka za Marekani wiki hii.

Marcel Malanga, Tyler Thompson, na Benjamin Zalman-Polun walikuwa tayari wamehukumiwa nchini DRC kwa kuhusika katika jaribio hilo lililofeli la mapinduzi lililotokea Mei 2024, ambapo watu waliokuwa na silaha walivamia makazi ya maafisa waandamizi wa serikali na kwa muda mfupi walikalia ofisi ya urais jijini Kinshasa.

Watatu hao waliachiliwa huru Jumanne katika makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, Massad Boulos, nchini DRC.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kutumia silaha za maangamizi, kulipua majengo ya serikali, na kupanga kuua au kuwateka nyara watu katika nchi ya kigeni.

“Washukiwa walipanga kwa makusudi, walichunguza maeneo ya mashambulizi, na waliwataja waathiriwa waliolengwa katika shambulio la kijeshi, wakiwa na nia ya kuua watu wengine, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu serikalini,” ilisema taarifa hiyo.

“Walihamasisha na kuwaajiri watu wengine kujiunga na mpango huo kama wapiganaji wa jeshi la waasi, na katika baadhi ya matukio, walitoa malipo ya kifedha kama kishawishi.”

Malanga, Thompson, na Zalman-Polun walikuwa miongoni mwa watu 37 waliohukumiwa na mahakama ya kijeshi ya DRC mnamo mwezi Septemba, wakipatikana na hatia ya kula njama ya kihalifu, ugaidi, na makosa mengine, na wote wakahukumiwa adhabu ya kifo.

Hata hivyo, mchakato wa kuwaachilia huru ulihusishwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini.

Watu hao watatu walikana mashtaka yote na walikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo bila mafanikio.

Wiki iliyopita, Rais Tshisekedi alipunguza adhabu yao hadi kifungo cha maisha, kabla ya kuwakabidhi kwa mamlaka za Marekani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI