Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App, Dodoma
WAKALA wa Vipimo (WMA) imenunua mita nne za mtiririko ili kuhakiki mita zilizofungwa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta, migodini, viwanja vya ndege, na maeneo mengine yanayotumia kasi kubwa ya kujaza mafuta. Lengo ni kuhakikisha mita hizo zinatoa vipimo sahihi vya kiasi cha mafuta.
Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, ameeleza hayo leo, Machi 25, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wakala hiyo katika miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
Amesisitiza umuhimu wa uhakiki wa mita hizo katika kulinda maslahi ya wauzaji na wanunuzi katika mnyororo wa usambazaji wa nishati ya mafuta.
Kihulla ameongeza kuwa WMA imefanikiwa kuhakiki matenki ya magari yanayobeba vimiminika kupitia kituo kikubwa cha uhakiki wa vipimo cha Misugusugu, ambacho kina uwezo wa kupima matenki ya malori 60 kwa wakati mmoja.
" Ongezeko la matenki yaliyohakikiwa limewezesha kuondoa kiasi kikubwa cha mafuta kwa haraka kutoka maghala na kusafirishwa nje ya nchi na mikoa mbalimbali.
Aidha, katika kuunga mkono kampeni ya nishati safi, WMA inaendelea kufanya ukaguzi na uhakiki wa vipimo kwenye mitungi ya gesi ili kuhakikisha wanunuzi wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha wanayolipa. Katika kipindi cha miaka minne, wakala imehakiki tani 958,593.17 za gesi zilizoshushwa na meli 210 nchini.
WMA inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi kwa kujenga na kukarabati ofisi, ikiwemo jengo la makao makuu lililopo Medeli, Mkoani Dodoma, lililogharimu bilioni 6.99.
Mwisho.
0 Comments