Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima APP DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema Serikali inatekeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea kwa kutoa ruzuku kwa wakulima wote na kwa mazao yote nchini.
Ameyasema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema tofauti na ruzuku zilizopita, katika awamu hii ruzuku ya mbolea inatolewa kupitia Mfumo wa Kidijitali wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System) ambao unatumika kusajili wakulima, waingizaji, wazalishaji na mawakala wa mbolea pamoja na kuratibu usambazaji na mauzo.
Amesema Matumizi ya mfumo wa kidijitali katika kusambaza mbolea ya ruzuku umeinufaisha Serikali hususani katika kuwezesha kuanzisha kanzidata ya kuaminika ya wakulima, Mawakala wa mbolea, Waingizaji na Wazalishaji wa mbolea Nchini.
"Mfumo huu wa kidijitali umekuwa nyenzo muhimu ya ufuatiliaji na uendeshaji wa biashara ya mbolea nchini kuanzia mbolea inavyoingizwa au kuzalishwa kwenye viwanda vya ndani hadi inapouzwa kwa mkulima katika maeneo mbalimbali nchini, " Amesema
Na kuongea "mfumo huu umerahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za matumizi ya mbolea nchini pamoja na kudhibiti udanganyifu katika mpango wa ruzuku ya mbolea, " Amesema.
Aidha amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, tasnia ya mbolea imeshudia ongezeko la aina za mbolea zinazopatikana sokoni na kuwapa wakulima fursa ya kuchagua mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na mazao wanayolima.
Ameeleza Katika kipindi hiki, mbolea zilizosajiliwa na kuruhusiwa kutumika nchini zimeongezeka kufikia 612 ikilinganishwa na mbolea 350 zilizokuwa zimesajiliwa mwaka 2020/2021.
Hata hivyo ameeleza katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.
Aidha amebainisha, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024, uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.
"Kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji nchini pamoja na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeshuduia kuongezeka kwa viwanda vya kuzalisha mbolea na visaidizi vya mbolea kutoka viwanda 16 mwaka 2020/2021 hadi viwanda 33 mwaka 2023/2024," Amesema.
Na kuongeza "Kati ya viwanda hivyo, vitatu (3) ni vikubwa, viwanda 11 ni vya kati na viwanda 19 ni vidogo, " .
Ndugu Waandishi wa Habari, katika kipindi cha Awamu ya Sita, Nchi imeshuhudia wawekezaji wakubwa walioonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea za Naitrojeni ambazo zinatumika kwa wingi kwa wakulima na pia zinatumika kama malighafi katika viwanda vilivyopo nchini.
" Wawekezaji hao tayari wamesaini Hati za Makubaliano kwa ajili ya kufanya uwekezaji, hatua ambayo haikuwahi kufikiwa kabla.
Kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini.
Amebainisha kuwa,matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024 ambapo ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.
"Lengo ni kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033 kwa kuzingatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024," Amesema.
Amesema kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 19,980,718 mwaka 2020/2021 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 14 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 128.
Mwisho.
0 Comments