Na Shomari Binda-Musoma
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma ( MUWASA) imeendelea na zoezi la kutoa elimu ya huduma za maji na kuwarudishia waliositishiwa bila kulipa faini.
Elimu hiyo inatolewa kwenye viwanja vya shule ya msingi Mukendo tangu machi 17 hadi 23 ikiwa ni wiki ya maji 2025.
Akizungumza na Matukio Daima kwenye banda la utoaji elimu lililopo kwenye uwanja huo leo machi 19, 2025 afisa wa MUWASA Joachim Saimon amesema moja ya elimu wanayoitoa ni wananchi kulinda upotevu wa maji.
Amesema mwananchi anayo nafasi ya kutoa taarifa juu ya upotevu wa maji pale wanapoona mivujo kwa kuwa mabomba yapo kwenye maeneo yao.
Joachim amesema wananchi wakiwa na elimu hiyo ya utoaji taarifa inakuwa rahisi kwa mafundi wa MUWASA kufika eneo la tukio na kufanya matengenezo
Amesema licha ya elimu hiyo kupitia Wiki ya Maji wanapokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma ya maji wanayoitoa.
Afisa huyo wa MUWASA amesema wanahakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi lakini kwenye kero na changamoto wanapokea maoni na ushauri na kufanyia kazi.
" Kupitia Wiki hii ya Maji tumesogeza huduma kwa wananchi hapa uwanjani kwa kutoa elimu kwa wananchi na kupokea kero kutoka kwenye mazingira yao.
" Hali ya upatikanaji maji ni nzuri hapa manispaa ya Musoma na wananchi wanafikiwa majumbani na hata wale wa viwandani ili kuweza kuwahudumia.
Amesema kupitia Wiki ya Maji wananchi waliositishiwa huduma ya maji wanayo fursa ya kurudishiwa maji pasipo kulipa faini ambayo mteja anadaiwa ikipewa ujumbe wa " Ofa ya Mama Samia Rudisha Huduma ya Maji bila Kulipa Faini"
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) mhandisi Nicas Mugisha amesema kupitia miaka 4 ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wananchi wanapata nafuu ya kurudishiwa maji kwa walisitishiwa pasipo kulipa faini.
Amesema MUWASA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ambayo serikali imeipatia fedha za kutosha.
Kwa upande wao wananchi waliofika kupata elimu wameishukuru MUWASA kwa elimu wanayoitoa kupitia wiki ya maji ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema " Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji"
0 Comments