Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinyijuma ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Muheza, Mkoani Tanga, amegawa hati 33 za mashamba ya Kwabada, katika shamba la Lewa, ambalo lilikuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu. Mgogoro huo umekuwa ukiendelea kwa takribani miaka 9 na leo umepatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa hati hizo, Mhe. Mwinyijuma alitoa shukrani za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kamishna wa Aridhi Mkoa wa Tanga, na kampuni ya Urasimishaji na Upimaji wa Ardhi, Ardhisol, kwa juhudi kubwa walizofanya kuhakikisha wananchi wa Kata ya Kwabada wanapewa hati zao.
“Mimi binafsi, nitowe shukrani zangu za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na kampuni ya Ardhisol kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Leo hii wananchi wa Kata ya Kwabada wanakabidhiwa hati zao, na binafsi nimejiskia faraja kubwa sana. Hii itapunguza migogoro ya ardhi kwa asilimia kubwa katika wilaya yetu ya Muheza, sambamba na Mkoa wetu wa Tanga,” alisema Mhe. Mwinyijuma.
Aidha, aliendelea kusema: "Hata hivyo, nisingependa kusikia matatizo ya ardhi yanaendelea hapa jimboni kwetu. Kesi nyingi ambazo zinaweza kumalizika haraka, hazipaswi kuwa na migogoro zaidi. Ni muhimu kumaliza migogoro ya ardhi haraka ili wananchi waweze kupata utulivu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dkt. Jumaah Mhina, alieleza: "Kile kinachofanyika hapa leo ni kuondoa wasiwasi na upotoshaji. Serikali imeamua kwa dhati kuhakikisha kuwa wananchi wanapata hati zao, na hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba maeneo haya yanatumika kwa maendeleo.
Mmoja wa wananchi waliokabidhiwa hati, Festo Kidumba, alisema: "Hii haikuwa kazi rahisi, lakini tumefanikisha. Tunashukuru kwa timu nzima ya Ardhisol na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa kufanikisha zoezi hili."









0 Comments