Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wameitaka Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuendelea kutoa Elimu kwa Wakulima juu ya upatikanaji wa pembejeo za Ruzuku zinatolewa na serikali ili waweze kunufaika nazo.
Aidha, wamesema serikali inawatambua wakulima hao na kuwataka Maafisa Ugani ngazi ya Kata kuendelea kutoa Elimu pamoja na kusajili wakulima wanaohitaji Pembejeo za mbegu na mbolea.
Akizungumza kwenye Mkutano Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Bariadi Mji, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, David Masanja amesema zoezi la kusajili wakulima linaendelea licha ya Kata zingine za Mjini Bariadi kutambulika kuwa hazina mashamba.
"Ningeomba Maafisa Ugani kwenye kata zetu kupitia Divisheni ya Kilimo, mfanye msukumo wa kuelimisha wananchi juu ya usajili wa wakulima wanaohitaji huduma...kata za mjini mnatambulika hamlimi, lakini zoezi hili lipo na pia tuelimishe wananchi kupitia mikutano ya hadhara sababu serikali imejipanga kutoa unafuu kwenye Ruzuku za mbolea na mbegu" amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Awali Diwani wa Kata ya Malambo, Kitebo Kulwa aliiomba Idara ya Kilimo kutoa ufafanuzi juu ya upatikanaji wa mbolea na mbegu za Ruzuku kwa wakulima wanaishi mjini wakati huo wanalima vijijini.
Ameeleza kuwa wakulima wamekuwa wakikosa huduma ya mbegu na mbolea za Ruzuku kwa madai kuwa wanatakiwa kuzipata kutoka kwenye maeneo wanayoishi ambayo ni mjini badala ya kuzipata vijijini ambako wanalima.
Akitolea ufafanuzi wa jambo hili, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Slivanus Gwiboha amesema amezunguka kata nyingi za Halmashauri hiyo kutoa Elimu na Bei elekezi ya mbegu na mbolea.
Amesema watahakikisha wanaendelea kupita kwa wakulima ili kutoa Elimu kwa usahihi na pia kutoa maelekezo ya maduka sahihi yaliyoidhinishwa na serikali kwa ajili kuwauzia wakulima mbegu za Mahindi ya ruzuku.
"Maelekezo yanasema, eneo unalolima ndipo utakwenda kupokelea Pembejeo zako kwenye Pamba iwe mbegu, dawa au vinyunyizi...kuna watu wanalima Gitoya, Maswa na maeneo mengine, Wana mgao wao kulingana na idadi ya ekari za eneo husika na ili kuleta usalama wa ugawaji wanatakiwa wakapokee kwenye maeneo wanayolima" amesema Gwiboha.
Mwisho.
0 Comments