Header Ads Widget

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YAIPONGEZA SERIKALI YA MKOA WA MARA

Na Shomari Binda-Musoma Matukio            Daima App

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imeipongeza serikali ya mkoa wa Mara kwa usimamizi wa fedha za ujenzi zinazoletwa na serikali kuu kwenye hospital ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Pongezi hizo zimetolewa leo machi 13,2025 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassan Selemani Mtenga baada ya kutembelea mkoa wa Mara na kufika kwenye hospitali hiyo.

Amesema serikali ya mkoa chini ya mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi imekuwa na usimamizi mzuri wa wakandarasi na fedha zinazoletwa na serikali kuona hospitali hiyo inakamilika na kutoa huduma ipasavyo.

Mtenga amesema Kamati imeridhishwa na ujenzi wa ukamilishwaji wa hospitali hiyo iliyoanza kujengwa toka mwaka 1976 na serikali ya awamu ya kwanza.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeleta fedha shilingi bilioni 4 za ukamilishaji na maendeleo ni mazuri ikiwemo usimamizi wa fedha.

" Tunaipongeza serikali ya mkoa kwa usimamizi mzuri wa fedha za ujenzi zinazoletwa kwenye hospitali hii ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

" Kikubwa ni serikali ya mkoa kuongeza nguvu ya usimamizi ili fedha zinazoletwa na serikali ya Mama Samia ziweze kukamilisha hospitali hii iweze kutoa huduma bora kwa wananchi",amesema

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Dkt.Christina Mnzava ameipongeza Wizara ya Afya na serikali ya mkoa wa Mara kwa maendeleo makubwa ya hospitali hiyo.

Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel amesema serikali ya awamu ya 6 imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya ambao unaonekana kwa macho na kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema kwa sasa idadi ya wagonjwa kutoka mkoa wa Mara kwenda hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mwanza imepungua kutoka wagonjwa 6400 hadi 900 katika kipindi cha mwaka 2024/2025

Awali akiikaribisha Kamati hiyo Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameishukuru serikali kwa kuleta fedha kwaajili ya ukamilishaji wa hospitali hiyo ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wa mkoa wa Mara.

Amesema hospitali hiyo kwa sasa imeanza kupokea wageni kutoka nchi jirani ambao wanafuata huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI