Header Ads Widget

'KUKOSEKANA KWA WELEDI KWENYE SEKTA YA HABARI KUMECHANGIWA NA KUCHELEWA KWA SHERIA MPYA YA HABARI'


NA MWANDISHI WETU.

Imepita miongo miwili sasa toka kuanza rasmi kwa mchakato wa ufuatiliaji wa sheria mpya ya habari ambayo imekuwa kilio kikubwa kwa kila aliye ndani ya sekta  hiyo adhimu, ambayo imekuwa muhimili mkubwa na kichocheo cha maendeleo ya wananchi. 

Zanzibar inatumia sera ya habari ya mwaka 2006 na Sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1997 ambayo inaenda kinyume  kwa baadhi vifungu na imetajwa kuzorotesha weledi kwenye sekta ya habari.

Miongoni mwa vifungu hivyo ni kifungu cha 30 cha Sheria ya Habari   ambacho kinampa mamlaka Waziri kuwa na mamlaka makubwa ya kufungia Gazeti bila ya kufuata mchakato wa Mahkama jambo ambalo linaathiri uhuru wa vyombo vya habari na kukosekana kwa weledi. 

Novemba 18, 2024 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika shamra shamra za miaka 4 ya Dk. Mwinyi aliulizwa hatua iliyofikiwa na serikali katika upatikanaji wa sheria mpya ya habari, alisema mchakato wa kupatikana kwa sheria mpya umefikia asilimia 80 na asilimia 20 zilizobaki zinatarajiwa kukamilika muda mfupi ujao. 

"Sheria ya habari imekuwa kiu kubwa kwa waandishi na wadau wa habari, niwahakikishie sheria mpya imefikia asilimia 80 na asilimia 20 zitakamilika muda mfupi ujao"- alisema Waziri Tabia. 

Baadhi ya waandishi wa habari wamenukuliwa wakisema Sheria ya mwaka 1988 imekuwa ikiwakwamisha katika utekelezaji wa majukumu yao kutokana na baadhi ya vipengele vinavyokandamiza haki na uhuru wa vyombo vya habari.

Mohammed Mazrui ni mwandishi mwandamizi wa habari, ambae pia ni mdau wa habari anasema kuchelewa kukamilika kwa sheria mpya ya huduma ya vyombo vya habari kwa namna moja au nyengine imechochea kuondoa weledi kwenye sekta ya habari huku akiongeza kwa kusema kuwa waandishi wamekuwa na hofu kuandika habari zinazohusu haki na wajibu kwa kukimbia kifungu cha 30 cha sheria kinachohalalisha kutokufatwa kwa taratibu za mahkama na mamlaka makubwa kupewa waziri jambo ambalo linanyonya huru wa habari nchini. 

"Sheria hii ya sasa imekuwa kikwazo kikubwa kwa waandishi kuhofia na kutotaka kugusa aina yoyote ya story zinazohusu haki na wajibu, naamini baada ya marekebisho ya sheria, Tasnia ya habari itazidi kukua na kuheshimika siku hadi siku"- alisema Mohamed.

Mwandishi wa habari Chipukizi kutoka Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Ummul-kulthum Abdallah amesema  sheria ya magazeti namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997 pamoja na sheria ya utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho ya sheria namba 1 ya mwaka 2010 zimeonekana kupitwa na wakati na zinahitaji marekebisho ya haraka ili kumpa nafasi mwandishi kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na uwazi zaidi.

Sheria hiyo inasema kuwa ‘Tume ina uwezo mkubwa wa kuthibiti maudhui /habari zinazotolewa na vyombo vya habari vya kieletroniki, hivyo nguvu hizo zinaweza kuathiri uhuru wa 18, vyombo vya habari katika utafutaji na usambazaji wa habari’

Amesema wao kama waandishi chipukizi hali hiyo inawanyima uhuru wa kupata habari na kupunguza weledi wa kazi na badala yake story zinazopewa kipaombele ni zile zilizoridhiwa na wahariri pamoja na viongozi wenyewe. 

Miongoni mwa matukio yaliyowahi kutokea hivi karibu yanayokandamiza uhuru wa vyombo vya habari kupitia kifungu namba 30  cha sheria ya habari, ni kufungiwa kwa chombo cha habari cha Bomba FM, Swahiba FM pamoja na vitisho kwa baadhi ya waandishi akiwemo Salma Said wa DW na Yassir Mkubwa  ambao wote hao, kimsingi walikua katika harakati za kuhabarisha jamii kuhusu ukweli, uwazi, haki na wajibu.

Wengine walliopata changamoto kupitia kifungu hicho ni vitisho kwa kituo cha habari cha Zenji FM na Mwandishi mwandamizi Ally Mohamed . 

Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji Zanzibar, Hiji Dadi Shajak amekiri kuwa muswada wa sheria ya huduma za habari ni ya muda mrefu na mchakato wake umekuwa ukileta matumaini ya kukamilika kwenye kipindi kifupi kijacho. 

"Jambo la sheria mpya ya habari kila mmoja anafahamu umuhimu wake na mchakato wake unazidi kuleta matumaini ya kwamba hivi karibu jambo hilo litakuwa ni historia hapa nchini"- alisema Hiji

Aidha wadau wa habari wamesema wataendelea kuwa tayari kutoa ushirikiano watakapohitajika kwa ajili ya kutimiza lengo hilo. 

Ni wajibu kwa mamlaka husika kuharakisha mchakato wa sheria mpya ya habari ili kunusuru kizazi cha sasa na baadae pamoja na kurudisha weledi kupitia sekta ya habari, ambao umeonekana kutoweka kadri siku zinavyokwenda mbele.

Ni matamanio ya kila mmoja mwaka huu wa 2025 ndio muda sahihi wa kuona lengo la kupatikana kwa sheria mpya iliyo rafiki kwa kila upande, linafikiwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI