Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Mohamed Kawaida, ameipongeza UVCCM Mkoa wa Singida kwa kutekeleza vyema sera ya Umoja wa Vijana na Uchumi Imara ya 2022/2027 kutokana na kuanzisha miradi.
Ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumzia na vijana wa UVCCM pamoja na viongozi wa CCM Mkoa wa Singida baada ya kuzindua fremu 73 za maduka ya kitega uchumi cha umoja huo na uzinduzi wa jengo la hosteli ya UVCCM katika Chuo cha St.Joseph tawi la Singida.
"Nimefurahishwa sana na jitihada zenu za kuhakikisha jumuiya inasimama na inajitegemea kiuchumi kama sera mahsusi ya UVCCM kwa mwaka 2022/2027 inavyoelekeza na ubunifu huu mlioufanya tunatamanj uwe mwanzo na sasa twendeni mbele tuachane na nyuma," amesema Kawaida.
Kawaida ametoa wito kwa mikoa yote UVCCM waanzishe miradi yao kulingana na jiografia ya maeneo yao ili kuifanya jumuiya hiyo inakuwa imara kiuchumi na kuachana na utegemezi.
Amesema UVCCM Mkoa wa Singida imekuwa ndio mfano wa kuigwa kwa kuanzisha miradi ya kiuchumi na kwamba mikoa mingine waige na waende kujifunza ili kila mmoja uwe na mradi wake wa kujitegemea na hivyo itakuwa imetekeleza sera ya Umoja wa Vijana na Uchumi Imara ya 2022 hadi 2027.
Kawaida amesema UVCCM ikijitegemea kiuchumi itakuwa na uwezo wa kueneza sera za chama kwa wananchi bila kumtegemea mtu na bila kuwa mtumwa wa mtu na pia viongozi wataweza kusimamia maamuzi yao sababu kiuchumi watakuwa vizuri.
Hata hivyo, ametahadharisha kuwa miradi hiyo inayoanzishwa na jumuiya hiyo isiwe sehemu ya kwenda kuwagawa bali iwe sehemu ya kwenda kuunganisha nguvu zenu na kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuifanya jumuiya iwe imara.
Aidha, amewataka vijana kuacha majungu na fitina kwasababu suala la kufanikiwa kupata uongozi haliji kwa wote kwa wakati mmoja bali linakuja kwa mtu mmoja mmoja na kwa awamu.
"Katika haya maisha hatuwezi kutoka wote kwa wakati mmoja lazima tukubaliane kutoka mmoja mmoja mfano Mhe.Halima ( RC Singida Halima Dendego) alikuwa na Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi UVCCM leo hii Dk.Nchimbi ni Katibu Mkuu wa CCM," amesema.
Kawaida amesema wale waliobahatika kupiga hatua wasiwacheke ambao hawajafanikiwa na badala yake wasaidie kuwavuta wafikie hatua ambayo wamefikia au zaidi na sio kuwakwamisha na kuwakatisha tamaa.
UCHAGUZI 2025
Kawaida akizungumzia kuhusu uchaguzi wa mwaka huu, amesema CCM ilishateua wagombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao wana sifa kubwa na ndio maana hadi sasa vyama vingine vya siasa vimeogopa na havijaweza kuteua wagombea wao hadi sasa.
Amesema UVCCM imejipanga kuhakikisha wagombea wote wa CCM kuanzia urais, wabunge na madiwani wanashinda uchaguzi wa mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba na kwamba muda utakapofika vijana watahakikisha wananadi sera za chama kwa nguvj zote ili wananchi waendelee kuichagua CCM.
Amesema ilani ya siasa ya 2025/2030 ambayo imeshaandaliwa ni nzuri sana na kwamba wananchi waisubiri wataona mambo mazuri yaliyomo humo.
UCHAGUZI MWENYEKITI UVCCM MKOA SINGIDA
Amesema baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida kuziba nafasi iliyokuwa wazi, vijana sasa waache walumbano na Singida sasa itulie.
Amesema vijana wampe ushirikiano Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida,Zulfat Mujja aliyechaguliwa ili umoja huo uendelee kustawi zaidi kwa maslahi ya chama.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Zulfat Mujja, ameahidi kushirikiana na vijana wa mkoa huu ili kuhakikisha jumuiya hiyo inakuwa imara.
MWISHO.
0 Comments